Mmepewa elimu ifikisheni kwa jamii

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewapa elimu waandishi wa habari nchini kutumia taaluma yao kuwa mabalozi wa kuelimisha umma kuhusu haki na huduma zinazotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), likisisitiza kuwa wanahabari ni daraja muhimu la kufikisha elimu kwa jamii.
Wito huo umetolewa na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya, wakati akifungua mafunzo kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanaoendelea na Kazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA), yaliyofanyika jijini Dar es Salaam kwa ufadhili wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).
Nyamhokya amesema waandishi wa habari wana nafasi ya kipekee ya kuwa kiungo kati ya taasisi za hifadhi ya jamii na wananchi, hivyo elimu wanayoipata kupitia mafunzo hayo itawawezesha kuripoti kwa usahihi na kuelimisha jamii kuhusu haki za wafanyakazi.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wanahabari wataweza kuelewa kwa undani huduma na mafao yanayotolewa na WCF, ikiwemo matibabu, fidia ya ulemavu wa muda na kudumu, malipo kwa wategemezi, huduma za utengemao pamoja na msaada wa mazishi kwa wafanyakazi wanaoathirika kazini.
“Waandishi wa habari ni daraja muhimu la kufikisha elimu kwa umma. Tunawategemea kuwa mabalozi wa kuelimisha wafanyakazi na waajiri kuhusu umuhimu wa WCF,” amesema Nyamhokya.
Aidha, ameitaka WCF kuendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi na wadau wa sekta ya habari ili kuongeza uelewa kuhusu mifumo ya fidia na kuhakikisha wafanyakazi wengi zaidi wananufaika na huduma hizo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA) Mussa Juma, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uelewa wa wanahabari kuhusu haki za kazi na ulinzi wa kijamii mahali pa kazi.
Amesema bado kuna changamoto ya wanahabari wengi kufanya kazi bila mikataba rasmi, hali inayowafanya kukosa baadhi ya haki za msingi kazini, hivyo elimu hiyo itasaidia kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya habari.
Naye Mkuu wa Mahusiano wa WCF Laura Kunenge amesema mfuko huo umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wafanyakazi nchini, hususan sekta ya habari, ili kuhakikisha wanapata uelewa sahihi kuhusu mfumo wa fidia na namna ya kuutumia pindi ajali au madhara yanapotokea kazini.
Amesema WCF itaendelea kushirikiana na taasisi za wafanyakazi na vyombo vya habari kuhakikisha elimu ya fidia inawafikia wafanyakazi wengi zaidi nchini, wakiwemo walioko kwenye sekta zisizo rasmi au zenye changamoto za mikataba.



