UN Tanzania kuweke nguvu ulinzi wa bahari

DAR ES SALAAM: UMOJA wa Mataifa (UN) nchini Tanzania umesema utaendelea kuunga mkono jitihada za serikali katika kulinda bahari, kusimamia taka kwa njia endelevu na kuimarisha sera bora za mazingira.

Hatua hiyo ni baada ya uzalishaji wa taka za plastiki kuongezeka nchini hivyo kupitia mashirika ya umoja huo, Tanzania itapata msaada wa kitaalamu na kifedha kuimarisha udhibiti na kuhifadhi rasilimali muhimu za baharini kwa kukabiliana na taka za plastiki.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwakilishi Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), Clara Makenya amesema tafiti zinaonesha kuwa zaidi ya tani milioni 11 za plastiki huingia baharini kila mwaka na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2040 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Takwimu za zinaeleza zaidi ya aina 800 za viumbe wa baharini wameathirika kutokana na uchafuzi huo, kwa kumeza plastiki, kunaswa katika taka hizo, au kupoteza makazi yao ya asili.

UN yaipongeza Tanzania uhuru wa vyombo vya habari

Amesema kati ya tani milioni 75 hadi 199 za plastiki zipo ndani ya bahari ulimwenguni kote na zimekuwa zikiathiri kwa kiasi kikubwa jamii za Pwani wakiwemo wavuvi wadogo na wanawake wanaotegemea bahari kwa maisha yao ya kila siku.
Ripoti ya UNEP inaeleza asilimia tisa pekee ya plastiki iliyowahi kuzalishwa ndiyo imeweza kurejerezwa upya hali inayoonyesha changamoto kubwa katika usimamizi.

Makenya ameeleza suala la kutokomeza taka za plastiki linahusisha wadau wote wakiwamo serikali, sekta binafsi na wananchi na kwamba hatua muhimu kupunguza taka hizo ni kuzirejesha upya kuwezesha kuwa na jamii iliyo salama, mazingira na bahari kwa vizazi vijavyo.

‘’Sekta binafsi inaweza kutengeneza ajira kwa kutumia rasilimali ambazo zitarejereza taka na hivyo zikatumika tena na hata wazalishaji waone namna ya kupunguza uzalishaji wa taka hizi ambazo zinaathiri mazingira yetu,’’ amesisitiza.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Shirika la Catholic Relief Services (CRS), Rose Mugashe amesema kama shirika wameanza program ya kulinda Ziwa Tanganyika ambalo linakabiliwa na uchafuzi wa mazingira, matumizi yasiyoendelevu na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema kwa kutumia programu hiyo, wanaweza kukuza uchumi, maisha endelevu na ushiriki wa jamii kulinda mazingira.

‘’Kampeni hii itahusisha wanawake, vijana, wavuvi na wakulima 119,000 Tanzania na Zambia kwa lengo la kuboresha ubora wa maji, kupunguza taka, kuongeza fursa za kiuchumi na maisha ya watu kwa kupata maarifa na zana za uendelevu wa taka,’’ ameeleza Mugashe.

Naye, Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi Mazingira (NEMC), Jamal Baruti amesema mwaka 2019 serikali ilitoa katazo la mifuko plastiki na kuainisha baadhi ya bidhaa kufungashwa kwa kutumia mifuko hiyo.

Amesema licha ya katazo hilo, taka za plastiki zimeendelea kuzalishwa kwa matumizi yasiyo sahihi na kwamba hutupwa kwenye mifereji ambayo hupeleka maji baharini hivyo kuathiri viumbe vilivyopo.

‘’Tunaendelea kutoa elimu kwa watu kuzingatia sheria bila kushurutishwa kuhusu matumizi ya mifuko ya plastiki na wanaokaidi kuwachukulia hatua ikiwemo kupigwa faini,’’ ameeleza Baruti.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button