Mapitio ya sera kusaidia walemavu vifaa vya teknolojia 2026

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema inafanya mapitio ya sera ya watu wenye ulemavu ya mwaka 1982 ili kujumuisha mambo mbalimbali ikiwemo kuwapatia walemavu vifaa tiba vya teknolojia saidizi kuanzia mwaka 2026.

Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Wambura Kizito amesema hayo wakati akizungumza kwenye Kongamano la kuadhimisha siku ya kimataifa ya teknolojia saidizi.

Ameeleza kuwa serikali imekua na mipango mbalimbali itakayowasaidia wananchi kuweza kumudu gharama za teknolojia saidizi ikiwemo kuhamasisha uzalisha wa hayo mahitaji hapa nchini hivyo mapitio ya sera hiyo yatatoa fursa kwa wahitaji kupata vifaa saidizi kwa unafuu.

Amesema takwimu za Sensa ya mwaka 2022 zinaonesha kati ya Watanzania milioni 61.7, watu milion 5.3 walitambulika kama watu wenye ulemavu ambao wapo katika makundi mbalimbali ambao wanatengeneza asilimia 11.2 asilimia ya watu wote nchini.

SOMA ZAIDI

Uzinduzi Sera ya Mambo ya Nje kuing’arisha Tanzania kimataifa

Mshauri Tiba wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dk Anthony Assey akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Balozi Dk Ulisubisya Mpoki alisema serikali inaendelea kutoa huduma za utengamao nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa teknolojia saidizi katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma za afya.

Alibainisha kuwa juhudi za serikali hivi sasa ni kuendelea na uboreshaji na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vinavyotoa huduma za utengamao ili kuwafikia watu wengi zaidi wenye ulemavu na wazee ambao ndiyo wanaohitaji huduma hizo.

‘’Vifaa na teknolojia saidizi huwezesha watu kuishi maisha yenye afya, ufanisi, uhuru na heshima zaidi, na kushiriki katika shughuli zao za maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jamii zao,’’alisema Dk Assey.

Dk Assey amesema kuna jumla ya watu bilioni 2.5 duniani wanaohitaji kutumia angalau aina moja ya kifaa au teknolojia saidizi, kama vile viti mwendo, vifaa vya kusaidia kusikia (shime sikio), miguu ya bandia, miwani au huduma za kidijitali.

Ameeleza kuwa licha ya kuwa na uelewa kuhusu upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi hapa nchini bado kuna ukosefu wa maarifa hasa kwa wananchi wanaoishi vijijini kuhusu namna na sehemu ya kupata huduma hizo.

Awali mkurugenzi wa Rehab Health, Remla Shirima alisema kongamano hilo limejikita katika kuimarisha huduma za utengemao na kuendeleza ushirikishwaji, ubora, ushirikiano, utu na ubunifu kupitia utetezi, kujenga uwezo, na ushirikiano.

Pia litaimarisha ushirikiano kati ya sekta mbalimbali ili kuboresha upatikanaji na ubunifu wa vifaa,kusaidia katika ujenzi wa mifumo jumuishi ya maendeleo na huduma za afya pamoja na kuchangia majadiliano ya kitaifa kuelekea kongamano la tatu la huduma za utengamao 2025.

Naye Mkurugenzi wa Kyaro Assistive Tech,Colman Ndetembea alisema taasisi hiyo inajihusisha na kubuni, kutengeneza, na kusambaza vifaa saidizi vinavyokidhi mahitaji ya jamii ya Kitanzania kwa kuunganisha teknolojia na ujuzi wa ndani.

Kongamano hilo lilikuwa na kaulimbiu isemayo ‘Fungua Maisha ya Kila Siku kwa Watu wenye Ulemavu’ iliyolenga kuwapatia nafasi ya kukaa pamoja kutafakari na kujadili umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya nchini ili kuongeza upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi kwa ajili ya kuboresha maisha ya walemavu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button