Uzinduzi Sera ya Mambo ya Nje kuing’arisha Tanzania kimataifa

UZI (Mei 19, 2025) Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024, ikiwa na mambo makuu sita.
Katika hafla ya uzinduzi huo Dar es Salaam, Rais Samia anasema mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje ya 2001 Toleo la 2024 ni matokeo ya mabadiliko na mageuzi ya kiuchumi yaliyotokea nchini katika kipindi cha miaka 24.
Anasema uwepo wa majanga ya afya na mabadiliko ya tabianchi, usalama wa nishati, uhalifu wa kimtandao na ugaidi unasababisha umuhimu wa sera hiyo kuwa ni hitaji la muhimu.
Kimsingi, uandaaji wa sera hiyo umefanywa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambayo kimsingi ndiyo wenye jukumu la kuandaa na kutekeleza sera ya mambo ya nje ili kulinda na kutetea masilahi ya taifa. Matokeo ya sera hiyo yanatokana na Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004 ili kuendana na mahitaji ya sasa.
Akizungumzia sera hiyo wakati wa uzinduzi wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo anasema imelenga kukuza diplomasia ya uchumi, kulinda maslahi ya taifa, kuendeleza uhusiano na nchi na taasisi mbalimbali na kuchangia amani na maendeleo duniani.
Anasema sera ya mambo ya nje ni mwongozo wa uhusiano wa kimataifa wa Tanzania unaolenga kulinda masilahi ya taifa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hii ni kwa kuzingatia misingi ya uhuru, haki za binadamu, demokrasia na ujirani mwema.
Anasema sera hiyo iliyoboreshwa mwaka 2024 inazinduliwa ikiwa inalenga mambo makuu sita. Jambo la kwanza ni kukuza diplomasia ya uchumi, kulinda na kutetea masilahi ya taifa, kuendeleza uhusiano na nchi na taasisi mbalimbali na kuchangia amani na maendeleo duniani.
Pili, ni kujenga mazingira wezeshi ya ndani na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, tatu ni kukuza diplomasia ya uchumi na nne ni kushughulikia masuala ya madeni. Mmengine ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda na
kimataifa pamoja na kudumisha misingi ya sera ya kutofungamana na upande wowote.
Aidha, anasema uboreshaji wa sera hiyo umetokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea duniani na kwamba kutokana na hali hiyo, serikali iliamua kuifanyia mapitio sera ya Mambo ya Nje kwa kushirikisha wadau mbalimbali kuhakikisha taifa linanufaika zaidi na uhusiano wa kimataifa.
“Mapitio ya sera hii yamebaini kuwa misingi ya sera bado inafaa, lakini kuna haja ya kufanya marekebisho ya mikakati badala ya kutunga sera mpya,” anasema Balozi Kombo. Anasema misingi ya sera hiyo imeonekana inakidhi mahitaji ya wakati ni wazi kuwa katika kutekeleza sera hiyo kulikuwa na manufaa ambayo nchi imenufaika nayo.
Anataja manufaa hayo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa ujirani mwema, ushirikiano wa kikanda na kimataifa, nafasi za uongozi katika taasisi za kimataifa na nchi kuwa mwenyeji wa taasisi za kikanda na kimataifa. Mbali na faida hizo, changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake ni uhalifu wa mipakani, uratibu wa mikataba ya kimataifa na ukosefu wa mwongozo wa kushirikisha diaspora wa Tanzania.
Changamoto nyingine ni kutotumika vya kutosha kwa lugha ya Kiswahili na kutojumuishwa ipasavyo kwa masuala ya mazingira na uchumi wa buluu.
Anasema: “Serikali ikaona kuna haja ya kuifanyia maboresho sera yetu ambayo yalilenga kuongeza uzingatiaji wa mila na katiba, kuweka mfumo wa uratibu wa mikataba, kushirikisha diaspora wa Tanzania, kutumia Kiswahili kama bidhaa na kuingiza masuala ya uchumi wa buluu, mazingira, jinsia na vijana.”
Baada ya kufanyiwa uboreshaji matokeo chanya yameanza kuonekana ambayo ni pamoja na kuongezeka kwa masoko ya nje, kuongezeka kwa watalii na kukua kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili. Mengine ni kuongezeka kwa Watanzania waishio nje, uchumi wa buluu, kuimarika kwa ujirani mwema, na kuwepo kwa mwongozo wa kushirikisha Diaspora wa Kitanzania walioko nje.
Kuhusu mkakati wa utekelezaji wa sera hiyo iliyoboreshwa, anasema utaainisha majukumu ya wadau mbalimbali wakiwamo sekta binafsi, mashirika ya kiraia, diaspora na wengine na utapitiwa kila inapobidi kwa mujibu wa mabadiliko ya mazingira.
Awali, Sera ya Mambo ya Nje ilijikita kutetea haki za wanyonge na kupiga vita ukoloni na ukoloni mamboleo, kupinga siasa za ubaguzi na ukandamizaji wa aina zote, kuendeleza Umoja wa Afrika na kuunga mkono sera ya kutofungamana na upande wowote.
Katika kuitekeleza, yapo mafanikio yaliyopatikana ambayo taarifa mbalimbali za wizara hiyo zimebainisha yakiwamo ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania.
Mafanikio yaliyoainishwa katika taarifa hiyo ya wizara ni pamoja na kulinda, kutetea na kudumisha uhuru; na mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, kutokomeza siasa za ubaguzi wa rangi Afrika Kusini na kujenga umoja na mtangamano wa kikanda na Bara la Afrika.
Inaelezwa kuwa mwaka 1990, msisitizo wa Sera ya Mambo ya Nje ulihuishwa na kujumuisha masuala ya kiuchumi na kijamii baada ya nchi nyingi barani Afrika hususani zilizopo Kusini mwa Afrika kupata uhuru na kukomeshwa kwa siasa za kibaguzi nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo sababu nyingine za kuhuisha sera hiyo ni kumalizika kwa vita baridi duniani na kuibuka kwa utandawazi na mageuzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Kwa kuzingatia mabadiliko hayo, mwaka 2001 serikali ilitunga sera mahususi kusimamia mambo ya nje iliyoendelea kubeba misingi ya kulinda uhuru wa kujiamulia mambo.
Misingi mingine ni kuheshimu mipaka ya nchi na uhuru wa kisiasa; kulinda uhuru, haki za binadamu, usawa na demokrasia; kukuza ujirani mwema, kuendeleza Umoja wa Afrika na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na wabia wa maendeleo.
Pia, kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa sera ya kutofungamana na upande wowote, kuimarisha ushirikiano na nchi zinazoendelea na kuunga mkono Umoja wa Mataifa na jitihada zake za kuimarisha maendeleo ya uchumi wa kimataifa, amani na usalama.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa sera hiyo ya mwaka 2001 iliweka bayana azma ya serikali kukuza uchumi na maendeleo ya taifa kupitia uhusiano wa kimataifa, msisitizo mkubwa ukielekezwa katika kutekeleza diplomasia ya uchumi.
Hivyo, jitihada za serikali zilielekezwa katika kuongeza wigo wa biashara kimataifa kupitia utafutaji wa masoko ya bidhaa mbalimbali za Tanzania nje ya nchi, kuvutia uwekezaji wa mitaji na teknolojia kutoka nje katika sekta za kijamii na kiuchumi na kutangaza vivutio vya utalii.
Pia, kuongeza fursa za ajira na masomo kwa Watanzania nje ya nchi na kushawishi upatikanaji wa misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Januari 14, mwaka huu Ikulu Dar es Salaam, Rais Samia aliandaa hafla ya sherehe za mwaka mpya kwa mabalozi na kuwaeleza moja ya mambo yatakayokuwemo kwenye Sera ya Mambo ya Nje iliyoboreshwa ni kuwapa hadhi maalumu, diaspora wa Kitanzania.
Hadhi hiyo itawawezesha kushiriki katika maendeleo ya Tanzania kwani kwa mujibu wa asiye raia wa Tanzania, anakosa haki za msingi zilizoainishwa kwenye Katiba hiyo ikiwa ni pamoja na umiliki na haki nyingine.
Akizungumzia tofauti ya Mtanzania na diaspora, Balozi Kombo anasema Watanzania wote waishio nje ya Tanzania ambao waliukana Utanzania wao na kupewa uraia wa nchi nyingine hao ndio diaspora na kuwa Watanzania waishio nje ambao hawajaukana uraia wa Tanzania wao ni Watanzania na si diaspora.
Uzinduzi wa sera hiyo unaendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa kwa kuweka mkazo katika diplomasia
ya uchumi, ulinzi wa maslahi ya taifa, ushirikiano wa kimataifa na ushawishi wa maendeleo jumuishi. Wadau mbalimbali wanasema ni wakati kwa Tanzania kuchukua nafasi yake kikamilifu duniani kwa kutumia sera bora na weledi wa kidiplomasia katika Karne hii ya 21.