Mgombea Isimani aahidi kusimama na wanawake

IRINGA: Mgombea ubunge wa Jimbo la Isimani kupitia chama cha UMD katika uchaguzi mdogo, Asma Othman, ameendelea kunadi sera zake kwa wananchi wa maeneo ya jimbo hilo huku akiomba kupewa ridhaa ya kuwaongoza na kuwatetea bungeni.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni katika kata ya Kising’a uliohudhuriwa na mamia ya wananchi, Asma amesema endapo atachaguliwa atahakikisha anasimamia maendeleo ya wananchi kwa kuweka mkazo katika sekta za afya, elimu, maji na uwezeshaji wa vijana pamoja na wanawake.

Amesema Jimbo la Isimani linahitaji uongozi unaoweka mbele maslahi ya wananchi na kusikiliza changamoto zao kwa vitendo badala ya ahadi zisizo na utekelezaji.

“Naomba kura zenu ili niwe sauti ya wananchi wa Isimani. Nitasimamia maendeleo na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa wakati,” alisema Asma.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo ameahidi kutetea haki za wanawake na watoto kwa kupigania upatikanaji wa huduma bora za afya, ikiwemo huduma za bure kwa wajawazito wakati wa kujifungua pamoja na huduma za matibabu kwa watoto wachanga.

Amesema wanawake wengi vijijini bado wanakabiliwa na changamoto za gharama za huduma za afya hali inayohatarisha maisha yao na watoto wao, hivyo ataweka msukumo mkubwa kuhakikisha huduma hizo zinaboreshwa na kupatikana kwa urahisi.

“Nitapigania haki za wanawake kupata huduma salama za uzazi bila vikwazo vya kifedha. Mama na mtoto wanapaswa kulindwa na kupewa huduma bora kwa sababu ndiyo msingi wa familia na taifa,” alisisitiza.

Habari Zifananazo

One Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button