‘Sote tuwe macho, tusiingie mtego wa adui’

DODOMA: WATANZANIA wametakiwa kuwa macho wasiruhusu misingi na nguzo ya Taifa itikiswe na kuingia kwenye mtego wa adui.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dk Mwiguku Nchemba, wakati anawasilisa makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2025/26.
“Nitoe rai kwa Watanzania wote tunaoipenda nchi yetu, tusiruhusu misingi na nguzo za Taifa letu zitikiswe na tusiingie kwenye mtego wa adui.
“Sote ni mashahidi kuwa mataifa yaliyowahi kuingia kwenye mfarakano kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na mizaha mizaha na kutokuheshimu misingi ya kitaifa, maneno ya rejareja yasiyo na ushahidi ya mtu mmoja mmoja, yasiyo na ushahidi kwa baadhi ya taasisi zisizo za serikali na yasiyo na ushahidi kwa baadhi ya vyombo vya habari.
“Mheshimiwa Spika, wakati mwingine uhalifu wa mtu mmoja mmoja au vikundi hujitokeza na kuwa tishio kwenye maisha ya kila siku ya wananchi. Ikumbukwe, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tatu walijitokeza wahalifu ambao walikuwa wanateka magari ya mizigo na mabasi ya abiria katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kukomesha uhalifu huo.
“ Aidha, katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne ulitokea uhalifu wenye sura ya ugaidi uliohusisha urushwaji wa mabomu kwenye nyumba za ibada, mikusanyiko ya watu na mashambulizi ya mtu mmoja mmoja wakiwemo watu wenye ulemavu wa ngozi. Tumesahau hili? Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kukomesha uhalifu huo.

“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, ulitokea uhalifu wa watoto kutekwa na kuuwawa, mtu mmoja mmoja kupigwa risasi kwenye makazi yake au katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Mtakumbuka, waliuwawa wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa wanaotokana na CCM na tulishuhudia pia miili iliyokuwa kwenye magunia na mifuko ikiwa imetupwa baharini. Na haya tumesahau? Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kukomesha uhalifu huo.
“Mheshimiwa Spika, hata sasa vimejitokeza viashiria vya uhalifu kama huo ambavyo havipiganwi kwa kupeleka vikosi na kampeni au kusema tunapigana vipi? Tukiendelea kunyoosheana vidole na kunyooshea vidole vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tutaacha adui aendelee na uhalifu.
“ Vita vya aina hii vinapiganwa kwa intelijensia, hivyo niwasihi watanzania wenzangu tuviache vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake na tuendelee kufanya kazi kwa maendeleo ya Taifa letu.
“ Mheshimiwa Spika, wakati mwingine uchochezi wa adui huwa ni kwa lengo la kuzifikia rasilimali nyingi au za kipekee zinazopatikana katika Taifa husika.
“Tunayo mifano yote ikiwemo ya mataifa yaliyokuwa na migogoro iliyochochewa na waliotamani kupora rasilimali hizo na pindi zilipoisha, migogoro nayo iliisha huku mataifa hayo yakiachwa masikini.
“Tumeshuhudia uchochezi katika mataifa mengine ukijipenyeza nyakati za uchaguzi kupitia wananchi kuchukiana wao kwa wao au wao na Serikali zao. Sote tuwe macho!!!.” Amesema Waziri Nchemba



