NGO’s Mtwara walalamikia upungufu wa wafadhili

MTWARA: MASHIRIKA yasiyo ya kiserikali (NGO’s) Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara yamelalamikia kupungua kwa wafadhili kutoka nje ya nchi hali inayopelekea kushindwa kutekeleza miradi kwa jamii.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya taasisi hizo leo Juni 13, 2025 wakati wa ghafla fupi ya jukwaa la NGO’s ngazi ya wilaya, Mkurugenzi wa Mtandao wa Mashirika hayo wilayani humo, Fidea Luanda amesema moja ya changamoto kubwa wanayopitia ni baadhi ya wafadhili kusitisha ufadhili katika mashirika au kubadili vipaumbele vya ufadhili.

“Kupitia changamoto hii tunatumia mbinu mbalimbali zikiwemo kutumia mapato ya ndani ya mashirika yetu, michango ya wanachama, kutumia wahisani wa ndani na mambo mengine,” amesema Fidea.

Jukwaa hilo limekutanisha zaidi ya mashirika 40 yanayofanyakazi zake katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara lengo likiwa ni kujadili mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2020/2021 na 2024/2025.

Serikali yasajili NGOs mpya 1,418

Naye, Msajili Msaidizi wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Manispaa ya Mtwara Mikindani, John Samo ametoa rai kwa mashirika hayo kuanzisha vyanzo vya mapato vitavyoiwezesha taasisi kufanya miradi kwa jamii na sio kutegemea mapato kutoka kwa wafadhili wa ndani au nje ya nchi.

Aidha, wilaya hiyo ina jumla ya mashirika yasiyo ya kiserikali 42 yanayotekeleza afua mbalimbali kama vile elimu, afya, kilimo, maji, mazingira, jinsia na gesi asilia yenye lengo la kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwatelea maendeleo wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanamtama Pole ametoa wito kwa baadhi ya mashirika yanayojihusisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia kuhakikisha wanayafikia makundi yote hususani watoto wa kiume ambao wapo katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button