Majaliwa ataka tafiti za tija mabadiliko sekta ya afya

DAR ES SALAAM: SERIKALI imetawaka watafiti na watunga sera kuwekeza katika tafiti zenye tija ili matokeo yake yatumike kutunga sera na mipango itakayoleta mabadiliko katika sekya ya afya.
Agizo hilo linaenda sambamba na wataalamu wa Tehama, afya na wasimamizi wa mifumo kuwekeza matumizi ya teknolojia katika kutoa huduma za afya ili kutambua na kuzuia magonjwa kupitia mifumo hiyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Juni 18, 2025 katika Kongamano la 13 la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) linalofanyika kituo cha magonjwa ya moyo Kampasi ya Mloganzila leo na kesho.

Majaliwa amesema ni maono ya serikali kuweka misingi imara kunufaika na teknolojia bila kuathiri ubora wa huduma, usalama na ulinzi wa taarifa na mikakati mizuri yenye yenye tija taifa.
“Kongamano hili basi likawe sehemu ya kutazama mafunzo, huduma, sera na miongozo ya teknolojia katika sekta ya afya, kuweza kubainisha mapungufu na kutengeneza mapendekezo kwa serikali na taasisi zote zinazohusika,”
“Kipekee zaidi, niwahimize muangalie ni namna gani tunaweza kuhakikisha mifumo yetu inayotumia teknolojia inawasiliana na ushiriki wa sekta binafsi na za umma unaongezeka ili kupeana uzoefu na hamasa,” amesema Majaliwa.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu, Wizara hiyo, Profesa Daniel Mushi amesema uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika chuo hicho unachochewa na matokeo chanya ambayo MUHAS imekuwa ikionesha katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Katika miaka ya hivi karibuni, chuo hiki kimefanikiwa kuingia miongoni mwa vyuo vitano bora katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ushahidi wa ubora wa mafunzo, tafiti zenye tija, na weledi wa hali ya juu wa wakufunzi wake,” amesema.
Amesema tafiti za MUHAS zimechangia kwa kiwango kikubwa kuibua na kuimarisha miongozo, sera, na mipango inayotekelezwa katika sekta ya afya na elimu.
“Haya yote ni matokeo ya kazi thabiti ya kitaaluma, ubunifu, na ushirikiano ndani ya jamii ya wanasayansi wa MUHAS,” ameongeza Prof Mushi.

Makamu Mkuu wa MUHAS, Appolinary Kamuhabwa amesema Katika kongamano hilo mawasilisho 200 ya tafiti yatafanywa kwa njia ya na mabango ambapo washiriki 218 kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Tanzania, Kenya, Marekani, Norway na Zambia ambao watatoa mawasilisho ya tafiti katika maeneo mbalimbali.
1.Magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea vya magonjwa,
2.Afya ya Mama, Mtoto na Kijana,
3.Tiba mbadala na tafiti za chanjo,
4.Afya ya kinywa, macho, masikio, pua na koo,
5.Akili mnemba, teknolojia na usalama na afya kazini, na
6.Utafiti wa mifumo ya afya na afya jumuishi.
Aidha amesema wasilisho kuu la kwanza lina kichwa cha habari; Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele kwa Bunifu na Tafiti kwa Kukabiliana na Changamoto Zinazobadilika za Afya Duniani” na litatolewa na Dkt. Nyanda Elias kutoka taasisi ya Taifa ya Tafiti za Tiba ya Binadamu (yaani National Institute for Medical Research – NIMR).
Wasilisho kuu la pili lina kichwa cha habari: “Kukabiliana na Uhalisia wa Magonjwa Mahututi Barani Afrika; Kuweka Kipaumbele kwa Mahitaji Muhimu ya Kujenga Mifumo Thabiti ya Afya.” ambalo itatolewa na Prof. Tim Baker na Dkt. Karima Khalid kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
“Mawasilisho yatakayofanywa hapa yanatokana na tafiti ambazo nyingi zimefadhiliwa na mashirika ya nje na kwa uchache wadau wa ndani. Tafiti hizi zinasaidia vyuo vikuu kuimarisha mchango wake katika kuleta mageuzi ya sera zetu na hatimaye uchumi wa nchi yetu kukua na kuimarika zaidi,”amesema Prof Kamuhabwa.



