Samia ametekeleza, aahidi neema zaidi Kanda ya Ziwa

RAIS Samia Suluhu Hassan ametekeleza moja ya ahadi yake kwa Watanzania aliyoitoa miaka minne iliyopita ya kukamilisha Daraja la JP Magufuli linalounganisha miji ya Kigongo na Busisi mkoani Mwanza.

Akihutubia wananchi waliofurika kushuhudia ufunguzi wa daraja hilo lililogharimu Sh bilioni 718, Rais Samia alisema mradi huo ni maono ya mtangulizi wake, Dk John Magufuli kukabili adha walizopata wananchi wa Kanda ya Ziwa.

Alisema kukamilika kwa daraja hilo kuna manufaa makubwa kwa wananchi, akigusia matumizi ya muda mfupi wa dakika nne kuvuka wakati kabla ya daraja, wananchi walitumia muda mrefu kuzunguka kufika upande wa pili.

“Daraja hili litakuwa alama ya nchi yetu na ni uthibitisho tumepiga hatua kubwa na kuifanya Tanzania kuwa taifa kubwa kiuchumi na ishara kuwa Tanzania sasa ina uwezo wa kupanga, kutekeleza na kufanikisha mipango mikubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa daraja hilo litakuwa ni kichocheo kizuri cha uchumi kutokana na kutumika pia na mataifa jirani hususani katika Kanda ya Maziwa Makuu.

Aidha, alisema kukamilika kwa daraja hilo kuna faida kubwa kiuchumi kwa sababu wananchi wataweza kusafirisha bidhaa zao kwa gharama ndogo tofauti na awali ambapo gharama zilikuwa kubwa.

Alisema daraja hilo ambalo gharama zake zimetokana na fedha za ndani kwa asilimia 100, limeondoa hatari iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kutumia usafiri usiokuwa na uhakika na hatimaye kupoteza maisha na mali zao.

Rais Samia alisema pamoja na kelele nyingi za kumkatisha tamaa katika kutekeleza mradi huo, aliamua kusimama imara kuhakikisha ndoto hiyo ya mtangulizi wake anaitimiza ili Watanzania waweze kufaidi kodi zao.

Alieleza kuwa daraja hilo linathibitisha kuwa Tanzania imekua kiuchumi na ni taifa linaloweza kufanya uamuzi wa mipango yake ya maendeleo bila kupata msaada kutoka nje.

Alisema ndoto ya Magufuli ilisababishwa na tukio lililompata wakati akienda kutoa posa kutoka Kigongo kwenda Busisi baada ya kufika ziwani na kukuta chombo kinachovusha watu si salama.

Aliamua kutumia baiskeli kuzunguka na alipofika alipata habari kuwa chombo kile kimezama na watu wote wamepoteza maisha.

“Jinsi shughuli za kiuchumi na kijamii zilivyokuwa zikiongezeka, mahitaji ya usafiri yaliendelea kuongezeka na ufanisi wa kiuchumi ulikuwa mdogo ikilinganishwa na mahitaji, ndiyo maana haishangazi kuona pamoja na kuwepo usafiri wa umma ilikuwepo mitumbwi na boti ndogondogo zilizokuwa zikitumika,” alisema Rais Samia.

Aliwaeleza Watanzania kuwa kumbukumbu zinaonesha kuwa kivuko cha kwanza kilinunuliwa mwaka 1968, kikiitwa Busisi Boat cha abiria 15. Mwaka 1971 ilileta kivuko cha MV Mwanza kinachobeba tani 20 na abiria 50.

Alisema vivuko vingine vilivyonunuliwa ni Geita Ferry (1972), MV Sabasaba (1977), MV Sengerema (1985), MV Misungwi (2008) na MV Mwanza (2018).

“Historia hiyo inaonesha jinsi serikali za awamu tofauti zilivyoguswa na kuwaletea wananchi usafiri wa uhakika ili waendelee kufanya safari zao,” alisema.

Vilevile, Rais Samia aliwahadharisha madereva watakaopita katika daraja hilo lenye urefu wa kilometa tatu, kuwa makini na kuchukua hadhari ili wasiliharibu daraja hilo kwa kuligonga.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button