Samia aomba machifu waliombee taifa

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka machifu, watemi na viongozi wa kimila kuombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu huku akikemea ramli chonganishi kwamba zinavunja amani kwenye uchaguzi.

Akizungumza kwenye tamasha la Bulabo la kabila la Wasukuma jana jijini Mwanza, Rais Samia alisema yeye kama Chifu Hangaya ameshapata baraka zote za kabila hilo kuelekea uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na anaamini machifu wengine wamembariki.

Alisema katika kipindi hicho cha uchaguzi, wapo wagombea wanaoomba kupata nafasi za kugombea kwenye uchaguzi huo watakaenda kwa waganga.

“Wanapokuja kwenu msifanye ramli chonganishi ndizo zinazovunja amani wakati huu wa uchaguzi. Akija na fungu lake kula, kama atashinda mwambie na kama hatashinda mwambie atashinda aende zake wewe kula chako,” alisisitiza.

Aliongeza: “Suala la kusema katibu wako hakupendi au kama hivi na vile hii si sawa, tunachotaka tumalize uchaguzi huu vizuri.”

Rais Samia alisema machifu wana jukumu la kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi huo kwa kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo.

Alieleza kwamba kwa kuwa machifu wana utaratibu wa kuchaguana kulingana na mila na desturi zao, utaratibu wa kikatiba unawapa fursa ya kuchagua viongozi kila baada ya miaka mitano.

“Nina ombi, ni ombi langu kwa machifu, watemi na viongozi wa kimila mliombee taifa letu uchaguzi ufanyike kwa amani,” alisema.

Pia, alisema alianza kuhudhuria Tamasha la Bulabo mwaka 2021 lakini kwa mwaka huu limetia fora kwani limekutanisha watu kutoka Oman na Afrika Kusini ambao machezo yao yanaendana na ya Kitanzania akimaanisha mila, desturi na tamaduni ni zilezile.

Aliagiza kuendelea kuenzi uhai wa tamaduni walizorithi kutoka kwa mababu sambamba na kuhifadhi tamaduni hizo kwa kizazi kijacho.

Alisema tamasha la kitaifa la utamaduni litafanyika mkoani Lindi na kwamba ni vema kuendelea kuyatangaza matamasha hayo na mengine kwa ajili ya kurithisha tamaduni na maadili.

Alisema taifa bila utamaduni ni mfu hivyo ni vema kutunza utamaduni na maadili yanayofaa kwa kuyarithisha kwa kizazi vijavyo ili Tanzania isiangukie kwenye taifa mfu.

Alisisitiza kwamba tamasha hilo litaendelea kuandaliwa na machifu na serikali itashiriki katika kukamilisha maandalizi chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kadhalika, aliahidi kufanya uboreshaji wa Uwanja wa Mpira wa Kisesa na kubariki kuitwa Chifu Hangaya kama ilivyoombwa na machifu hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi alisema serikali ina mkakati wa kulifanya tamasha hilo kuwa urithi wa dunia.

Alisema wameanza mchakato wa kufanya utafiti wa kuhifadhi tamaduni  huo kwenye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kuanzia Machi mwakani.

Alisema lengo ni kufanya utamaduni huo kuwa urithi usiofutika wa dunia sambamba na kuenzi na kulinda utamaduni

“Sherehe za Bulabo hufanyika wakati wa mavuno na huenda sambamba na Sikukuu ya Ekaristi kwa imani za Wakatoliki ambao wametamadunisha utaratibu huu nasi tumeona vema kulifanya urithi wa dunia,” alisema.

Profesa Kabudi alisema wameanza utafiti wa lugha zote na idadi ya watu wanaozungumza kwa lengo la kukuza misamiati na istilahi pamoja na kuongeza lahaja zote zinazozungumzwa na nchi jirani.

Alisema pamoja na Tanzania kuwa na utofauti mkubwa wa lugha, imeonesha mshikamano kuliko nchi nyingine.

Kadhalika, alisema serikali ina mkakati wa kujenga jengo la utamaduni jijini Dodoma ambalo litakuwa na ofisi za viongozi wa kimila na maeneo ya kuhifadhi vifaa vya kijadi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button