Serikali: Chadema bado ina nafasi uchaguzi 2025

MWANDISHI Mkuu wa Sheria, Onorius Njole amesema Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA) bado kina nafasi ya kusaini Kanuni za Maadili za Uchaguzi Mkuu 2025 kabla ya mchakato wa uteuzi wa wagombea haujaanza.

Alisema kanuni hizo hazijaanza kutumika na kufanya kazi rasmi hivyo Chadema wanayo fursa ya kusaini kanuni hizo zitakazoanza kutumika siku moja kabla ya uteuzi wa wagombea.

Njele alitoa ufafanuzi huo jana wakati wa kongamano la kitaifa la sheria lililolenga kujengea uelewa wa wananchi juu ya marekebisho ya sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

“Chadema wanayo nafasi kabla mchakato haujaanza kanuni zipo wazi na zinaanza kutumika siku moja kabla ya uteuzi wa wagombea,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Mawakili wa Serikali, Ado November alisema serikali imefanya maboresho katika sheria za uchaguzi hivyo asitokee mtu akaongelea kuwa serikali haijafanya uboreshaji wowote.

Alisema mojawapo ni uwepo wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ambayo imeshatungiwa sheria yake sambamba na mapendekezo ya kesi zinazohusu uchaguzi kukamilika ndani ya miezi sita.

Uboreshaji mwingine ni kuondoa mamlaka ya wakurugenzi wa manispaa kusimamia uchaguzi mkuu na sasa jukumu la kusimamia uchaguzi litafanywa na watumishi wa umma waandamizi wenye sifa na vigezo watakaosimamiwa na Inec.

Wakili wa Kujitegemea, Francis Stolla alisema Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi 2024 imeipa uhuru tume wa kufanya uteuzi wa wajumbe wa tume ya taifa ya uchaguzi kwa kufanya usaili kabla ya kupendekeza majina kwa Rais.

Alisema kamati hiyo imeundwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wajumbe wengine kuteuliwa kutokana na maombi ya wananchi kupitia tangazo lililotolewa katika magazeti.

Imefanya uboreshaji mwingine pia ambao ni wafungwa kupata nafasi ya kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais.

Alisifu kuwa mchakato huo ni wa wazi ambao awali haukuwepo. Aliwataka wananchi kupuuza upotoshaji unaoendelezwa na baadhi ya watu.

Alisema serikali imeendelea kuboresha sheria hivyo Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utafanyika bila kikwazo chochote.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button