Mazishi ya Egdar Lungu yakwama

JOHANESBURG : MAHAKAMA nchini Afrika Kusini imezuia kufanyika kwa mazishi ya faragha ya Rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu, yaliyopangwa kufanyika leo mjini Johannesburg.

Uamuzi huo umetolewa muda mfupi kabla ya kuanza kwa ibada ya mazishi ya kiongozi huyo, kufuatia mvutano wa muda mrefu kati ya familia yake na serikali ya Zambia.

Taarifa zinaeleza kuwa serikali ya Zambia inasisitiza Lungu azikwe kitaifa nchini humo, kwa heshima ya nafasi yake ya uongozi aliyoishika kati ya mwaka 2015 hadi 2021.

Hata hivyo, familia ya Lungu inapinga hatua hiyo wakidai kuwa hali ya kisiasa nchini humo, hasa uhusiano mbaya kati ya Lungu na Rais wa sasa, Hakainde Hichilema, ndiyo sababu kuu ya msimamo wao wa kutaka mazishi yawe ya faragha nje ya nchi.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, wanandugu wa Lungu waliwasili mahakamani mjini Pretoria wakiwa wamevalia mavazi meusi ya maombolezo na kutoa hoja za kutaka kiongozi huyo azikwe kwa utaratibu walioupanga, wakisisitiza kuwa ni maamuzi ya familia kulingana na matakwa ya marehemu.

Edgar Lungu alifariki dunia Juni 5 mwaka huu katika hospitali moja mjini Johannesburg kutokana na ugonjwa ambao haukuwekwa wazi na familia.

Rais huyo wa zamani wa Zambia , alikuwa na umri wa miaka 68 wakati wa kifo chake na amekuwa akiishi Afrika Kusini tangu aondoke madarakani mwaka 2021.

Tayari Serikali ya Zambia imeeleza dhamira yake ya kutuma maombi rasmi ya kurejeshwa kwa mwili wa Lungu nyumbani kwa maziko ya kitaifa, hatua ambayo sasa inaonekana kuingia kwenye mzozo wa kisheria kati ya pande hizo mbili.

Hali hiyo imesababisha sintofahamu kuhusu hatma ya mazishi ya kiongozi huyo wa zamani. SOMA: Balozi Luteni Jenerali Mkingule asaini maombolezo ya Dk Lungu

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button