Ukraine kujiondoa kwenye Mkataba wa Ottawa

KYIV, UKRAINE : RAIS wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, ametia saini amri ya kuiondoa rasmi nchi yake kutoka kwenye Mkataba wa Ottawa wa mwaka 1997, unaopiga marufuku matumizi, utengenezaji, usafirishaji na uhifadhi wa mabomu ya ardhini.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Zelenskyy amesema utekelezaji huo unatokana na uamuzi wa Baraza la Usalama na Ulinzi la Kitaifa la Ukraine uliotolewa Juni 29, 2025, unaoelekeza nchi hiyo kujiondoa kwenye mkataba huo.
Hata hivyo, amri hiyo haitaanza kutekelezwa hadi iidhinishwe na Bunge la Ukraine na baadaye kuwasilishwa rasmi kwa Umoja wa Mataifa. SOMA: Marekani, Ulaya, Ukraine kujadili mzozo wa Urusi
Ukraine inaungana na baadhi ya nchi jirani za Ulaya Mashariki, zikiwemo Poland na mataifa ya Baltic, ambazo tayari zimechukua hatua kama hiyo, zikieleza kuwa ni njia ya kujilinda kutokana na ongezeko la vitisho vya kijeshi kutoka kwa Urusi.
Mkataba wa Ottawa uliosainiwa mwaka 1997, uliwekwa kwa lengo la kulinda raia dhidi ya madhara ya mabomu ya ardhini, ambayo mara nyingi huendelea kuwa tishio kwa maisha hata baada ya vita kumalizika.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Urusi imeendeleza mashambulizi ya kijeshi nchini Ukraine na kuteka baadhi ya maeneo, hali inayosababisha mabadiliko ya mikakati ya kiusalama kwa serikali ya Kyiv.



