Rwanda, DRC simamieni mkataba wa Washington kudumisha amani

WIKI iliyopita dunia ilipata habari za kutia moyo na zenye matumaini ya kuufikisha mwisho mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mgogoro huo uliodumu kwa miaka zaidi ya 30, umeteketeza maisha ya maelfu ya wananchi wa taifa hilo kubwa zaidi barani Afrika na kusababisha janga kubwa la wakimbizi duniani.

Asilimia kubwa ya wakimbizi waliotokana na mzozo huo wapo katika mataifa ya Burundi, Tanzania, Uganda na Rwanda na Umoja wa mataifa umekuwa ukitumia fedha nyingi pamoja na nchi wenyeji kugharamia mahitaji ya wakimbizi hao.

Wiki iliyopita habari nzuri zilisikika kutoka nchini Marekani ya kufikiwa makubaliano kati ya Rwanda na DRC kumaliza kabisa mapigano na kurejesha amani ya kudumu Mashariki mwa taifa hilo.

Habari za kufikia muafaka wa amani zimehitimisha historia mbaya, ukatili, unyanyasaji na ubakaji wa wananchi wa DRC na kuwalazimisha kuyakimbia makazi yao na kuishi ukimbizini bila kujali rika.

Tumefurahishwa na ushiriki wa taifa kubwa la Marekani ambalo kila mtu anaamini kuwa linaweza kukemea kinachoendelea Goma na Kivu na kusikilizwa na kutekelezwa.

Hivyo, tunaamini mkataba huo uliosainiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa pande zote utadumu ikiwa pande zote mbili zitautekeleza kwa nia ya dhati kwa maslahi ya wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wengi wao tangu wazaliwe hawajawahi kuona amani ikitamalaki nchini kwao.

Mkataba huo uliopewa jina la ‘Mkataba wa Washington’ ulizaliwa kutokana na mazungumzo yaliyosimamiwa na Marekani na Qatar kwa lengo la kumaliza mgogoro huo ili kuruhusu makampuni makubwa ya Marekani kuja kuwekeza.

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe pamoja na wa DRC Thérèse Wagner waliwawakilisha wakuu wa nchi zao ambao ni Paul Kagame na Felix Tshisekedi kusaini makubaliano hayo mbele ya Rais Donald Trump na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Marco Rubio.

Tunampongeza Rais wa Marekani, Donald Trump kwa kukusudia kuumaliza mgogoro huo ambao umekuwa kero namba moja barani Afrika na nchini DRC kwa ujumla.

Kutokana na nia ya dhati ya Rais Trump ya kuleta amani ya kudumu, tunazisihi nchi husika zilizotia saini kumaliza mgogoro huo kuwa mkataba huo unahitaji kutekelezwa kikamilifu ili kuhakikisha kuwa amani ya kudumu inarejea.

Tunaungana na wapenda amani wote Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla kuzitakia heri nchi zilizotia saini mkataba huo na kuziomba zijielekeze katika kutekeleza matakwa ya mkataba.

Tunaiomba Marekani kuhakikisha inasimamia ahadi ya Rais Trump ya kuwa yeyote atakayekwenda kinyume na mkataba husika atachukuliwa hatua za kisheria na kwamba vikwazo vya kiuchumi vitahusika kwa yeyote atakayeirudisha DRC katika machafuko hayo.

Ni matumaini yetu kuwa katika utekelezaji wa mkataba huo, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) itashiriki na kutoa mchango wake mkubwa wa kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa na mkataba unaendelea kutekelezwa kikamilifu na pande zote.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. I am now making an extra $19k or more every month from home by doing a very simple and easy job online from home. sxs I have received exactly $20845 last month from this home job. Join now this job and start making extra cash online by following the instructions on the given website………………….. ­­W­­w­­w­­.­­J­­o­­i­­n­­S­­a­­l­­a­­r­­y.­­­C­­­o­­­m­­­

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button