Miaka 10, kilimo, uchumi waimarika

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ambapo sekta ya kilimo imeendelea kuwa uti wa mgongo wa mafanikio hayo.

Kilimo chazidi Kung’ara

Takwimu zinaonesha kuwa tangu mwaka 2014/15, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani 16,015,238 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2024/25. Ongezeko hili la asilimia 33 limepelekea ongezeko la utoshelevu wa chakula kutoka asilimia 125 hadi 128.

Biashara ya mazao kupitia mfumo rasmi wa ushirika nayo imeimarika kwa kasi. Mauzo ya mazao hayo yameongezeka kutoka tani 591,268.12 mwaka 2021 hadi tani milioni 2.23 mwaka 2025. Thamani ya mauzo imepanda kutoka TZS trilioni 1.1 hadi TZS trilioni 4.2. Vilevile, uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 200,000 hadi 528,262 katika kipindi hicho.

Bajeti yapanuka, huduma zaboreshwa

Serikali imeongeza bajeti kutoka TZS trilioni 34.86 mwaka 2021 hadi TZS trilioni 50.29 mwaka 2025. Kupitia ongezeko hilo, huduma muhimu zimeimarika ikiwemo upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, huduma za maji na umeme katika maeneo ya mijini na vijijini, elimu bure na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.

Uchumi wakua zaidi ya wastani wa Afrika

Tanzania pia imeonyesha ukuaji wa kiuchumi wa kuvutia. Kwa mujibu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.5 mwaka 2024 kutoka asilimia 3.9 mwaka 2021. IMF inakadiria kuwa ukuaji huo utafikia asilimia 6 mwaka huu, ukizidi wastani wa dunia wa asilimia 2.3 na ule wa Afrika wa asilimia 4.

Pato la taifa limepanda kutoka TZS trilioni 156.4 mwaka 2021 hadi TZS trilioni 205.84 mwaka 2024. Aidha, pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka TZS 2,397,411 mwaka 2020 hadi TZS 2,938,634 mwaka 2024.

Uwekezaji waongezeka, ajira zazalishwa

Katika jitihada za kuvutia uwekezaji, Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza mageuzi ya kisera kwa kufuta kanuni 66 na kupunguza jumla ya tozo, ada na faini 383. Hatua hizo zimechangia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kusajili miradi 2,175 yenye thamani ya USD bilioni 25.53. Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja 650,674 kwa Watanzania.

Maji kwa maendeleo

Sekta ya maji pia imenufaika na ongezeko la bajeti. Serikali imeanzisha miradi 28 mikubwa yenye thamani ya TZS trilioni 1.3 ambayo imewanufaisha zaidi ya wananchi milioni 5.9. Mojawapo ya miradi hiyo ni Bwawa la Kidunda, ambalo linatarajiwa kuhifadhi lita bilioni 190 za maji. Ujenzi wa bwawa hilo umefikia asilimia 29.

Hifadhi ya jamii yaimarishwa

Kwa upande wa hifadhi ya jamii, serikali imeongeza malipo ya mkupuo wa mafao kutoka asilimia 33 hadi 40. Pia, kima cha chini cha pensheni kwa mwezi kimeongezwa kutoka TZS 100,000 hadi TZS 150,000, hatua inayolenga kuboresha maisha ya wastaafu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button