Muhas yatoa elimu sabasaba huduma za dharura

DAR ES SALAAM: WATANZANIA wanaendelea kuelimishwa namna ya kukabiliana na huduma za dharura kwa wagonjwa wanaokutana na changamoto mbalimbali za kiafya, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura wa Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) anaeleza.
Dk Evelyne Mapunda ametoa kauli hiyo leo Julai 1, 2025 akiwa katika banda la MUHAS viwanja vya Sabasaba vilivyopo wilaya ya Temeke ambapo mwandishi wa mtandao huu alitaka kujua kwa kiasi gani wamejipanga kutoa elimu, huduma ushauri kwa wananchi kuhusu afya.

Vifaa mbalimbali vya teknolojia vinavyotumika kutoa mafunzo na huduma za afya za dharura, ambapo mafunzo na huduma zinatolewa viwanja vya sabasaba na Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)
Akizungumza na HabariLeo, Dk Evelyne amesema kwa anayetoa huduma ya dharura anapaswa kuwa na ujuzi wa kiwango Fulani hivyo wamejikita kutoa elimu hiyo ili kuwasaidia wananchi wanapokutana na changamoto hizo.

“Mfano umekutana mtu amepata jeraha kutokwa na damu kwa wingi au kwa mtu aliyepata degedege, ni huduma gani za awali anapaswa kufanya hivyo tunatoa huduma za aina hiyo pia,” amesema Dk Evelyene.
Amesema kupitia maonesho hayo wamejikita pia kufanya uchunguzi wa magonjwa ya kinywa na meno na watakaobainika kuwa na changamoto kubwa watapewa maelekezo maalumu.

Fredrick Andrew, Daktari wa kinywa na meno, MUHAS pembeni akiwa na kiti cha kutolewa huduma ya kinywa na meno viwanja vya sabasaba.
Amesema wananchi wanaridhishwa na huduma hizo hasa baada ya kupewa elimu ya kutosha maalum namna ya kuzuia magonjwa yatokanayo na kinywa na meno.
“Tunawashauri dawa gani ya kutumia, mswaki na namna ya kusafisha meno yao, na matumizi ya vyakula mbalimbali ambavyo vinaweza kusababisha kutoboka kwa meno kama vyakula vyenye sukari tunashauri,” amesema Dk Andrew.

Huduma mbalimbali za uchunguzi wa kimywa na meno zikiendelea
MUHAS pia imeweka kambi kutoa elimu kuhusu huduma za uuguzi na ukunga ambapo wamekuwa wakionesha teknolojia mbalimbali zinavyofanya kazi kwa watoto wenye changamoto ya kupumua na kuzalisha wajawazito.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkufunzi Msaidizi kutoka MUHAS, Hamza Lilenga amesema wananchi waofika katika banda lao wamekuwa wakielimishwa na kuona namna vifaa vya kisasa vinavyofanya kazi kwa ufanisi hospitalini.



