CCM yafunga pazia leo, Sabaya achomoza

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuomba uteuzi katika nafasi za ubunge, uwakilishi, na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Kuanzia Juni 28, mwaka huu hadi leo saa 10:00, wanaCCM hao walikuwa katika uchukuaji na urejeshaji wa fomu ulioshuhudia ‘mafuriko’ katika ofisi zao zilizowekwa maalumu kwa kazi hiyo kabla ya kuanza kwa vikao vya uteuzi.

Kwa mwaka huu, vikao hivyo vya uteuzi vitaanza katika ngazi za awali hadi kufikia katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo itafanya uteuzi wa mwisho, kabla ya wajumbe kupigia kura wenzao wasiopungua wanne kupata wawakilishi wao katika kupambana na vyama vya upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

Hadi jana uchukuaji fomu ulikuwa unaendelea, na katika majimbo ya Wilaya ya Temeke walikuwa wamejitokeza 57 wakiwemo 23 katika Jimbo la Temeke. Katika Jimbola Mbagala waliochukua ni 22 wakati Jimbo la Chamazi walikuwa 12.

Katibu wa CCM wa Wilaya, Daniel Sayi aliwataja baadhi ya waliochua fomu Temeke ni Doroth Kilave anayeomba tena ridhaa, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kisangi, Benard Mwakyembe, mdau wa mpira wa miguu; Shafii Dauda na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Abdallah Mtolea.

Sayi alisema kwa Jimbo la Mbagala waliochukua fomu ni aliyekuwa Meya wa Temeke, Abdallah Mtinika, Dk Elisha Osaki, Dk David Gululi, Amina Battasi, Lilian Mzava, Seif Sulle, Siagi Kiboko, Naanya Maanya, Poster Mahaba na Masudi Kandoro.

Kwa Jimbo la Chamazi aliwataja Abdallah Chaulembo, Melchizedek Hango, Ami Kitambulio, Zuhura Khalfan, Denis Mrisho, Tom Mkenda, Mariam Kambi, Mohamed Lubavu, Munir Taib na Hopetatus Kaijage.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Ilala, Sylivester Yaledi alisema katika wilaya hiyo yenye majimbo manne ya Kivule, Segerea, Ilala na Ukonga, watia nia 59 wamechukua fomu hadi kufikia Julai 1.

Akifafanua idadi hiyo, Yaledi alisema katika jimbo jipya la Kivule watia nia 33 wamejitokeza kuchukua fomu na hadi sasa wanaendelea kurejesha.

Katika Jimbo la Segerea waliojitokeza kuchukua fomu ni watia nia 11 akiwamo mbunge anayetetea jimbo hilo Bonnah Kamoli. Wengine ni Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Rajabu Amiry na kada Masele Masunga.

Katika Jimbo ya Ilala watia nia 11 wamejitokeza akiwamo mbunge wa sasa Mussa Azzan Zungu ambaye ni Naibu Spika, huku Ukonga wakijitokeza watano akiwamo mbunge wa sasa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.

Katika Wilaya ya Kinondoni yenye majimbo mawili watia nia 38 wamechukua fomu. Katika Jimbo la Kawe ushindani umeonekana huko baada ya wagombea 25 kujitokeza akiwemo Magige Nyerere mtoto wa tatu wa wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Gaston Francis, Geofrey Timoth, Maria Sebastian, Furaha Dominic, Hemed Nkunya na Justine Maniula.

Katika Jimbo la Kinondoni watia nia 13 wamechukua fomu akiwamo Abbas Tarimba, Idd Azzan na Wilfred Nyamwiga huku vijana nao wakijitokeza kwa wingi. Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amechukua fomu Jimbo la Arumeru Magharibi akiwa miongoni mwa wanachama 20.

Sabaya amechukua fomu ofisi za CCM jimboni humo mkoani Arusha akiongozana na mkewe Jesca Thomas, na kusema anamwachia Mungu afanye kazi yake. Jimboni Longido wanaCCM sita wamechukua fomu akiwemo mbunge wa sasa Dk Steven Kiruswa, Lairumbe Laizer, Nicholaus Senteu na Martha Ntaipo.

Kwenye Jimbo la Ngorongoro hadi Julai 1 wamechukua tisa akiwamo Joseph Parsambei, Valentino Ngorisa na Silyvanus Pinda. Monduli pia wako tisa ambao ni Paul Mollel, Biliuda Kisaka, Daniel Porokwa, Shaban Adam, Preygod Munisi, Fred Lowassa (mbunge wa sasa), Isack Joseph, Sakaya Kabuti, na Mwenyekiti wa CCM Monduli, Wilson Ole Lengima.

Hadi jana wanaCCM 13 walikuwa wamechukua fomu katika Jimbo la Arusha Mjini. Kibaha Mjini wako Abubakar Allawi, mbunge wa sasa Silvestry Koka, Mussa Mansour, Margareth Mwihava, James Deogratias, Fadhil Hezekiah na Hamza Chambusa.

 

 

 

Imeandikwa na Rehema Lugono na Shakila Mtambo (Dar) na John Mhala (Arusha)

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button