Uganda yajiunga rasmi na BRICS

KAMPALA : UGANDA imejiunga rasmi kama mshirika wa jumuiya ya BRICS inayojumuisha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia bila masharti ya kisiasa kutoka mataifa ya Magharibi.
Kwa miaka mingi, Uganda imekuwa ikitegemea wafadhili wa Magharibi hususan katika sekta ya afya, lakini masharti kuhusu haki za binadamu na utawala bora yamekuwa kikwazo. Ushirikiano na Urusi na China unachukuliwa kuwa nafuu zaidi, kwa sababu hauhusishi masharti hayo.
Urusi imeanza kuiunga mkono Uganda kwa kutoa msaada wa kijeshi ikiwemo vifaa vya ramani za kisasa vyenye thamani ya Dola milioni 3, huku ikiahidi kushirikiana katika sekta nyingine kama kilimo na nishati ya nyuklia.
Katika afya, Urusi inaongeza ushiriki wake baada ya baadhi ya misaada ya Marekani kusimamishwa. Uganda inatarajia kupata msaada wa vifaa tiba, mafunzo ya wataalamu, na ujenzi wa miundombinu ya afya kupitia ushirikiano huu mpya.
Wataalamu wanasema Uganda inapaswa kutumia fursa hii kupanua wigo wa ushirikiano bila kutegemea upande mmoja. Ushirikiano na BRICS unaweza kusaidia kukuza uchumi, lakini lazima ujikite katika manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.
SOMA: BRICS yapingana na ushuru wa Trump



