Hotuba ya kihistoria bungeni
NI hotuba itakayokumbukwa kwa muda mrefu na Watanzania na wafuatiliaji wa siasa za Tanzania hasa kutokana na ukweli kuwa, ilikuwa ‘imeshiba’ na imebeba kila kitu alichoahidi na amekitekeleza.
Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kuhitimisha shughuli za Bunge la 12 Dodoma Juni 27, 2025, imekuwa ya kihistoria kwa sababu nyingi.
Kwanza, imechukua muda mrefu, dakika 166 huku Rais Samia ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu aliyeingia bungeni baada ya kukagua gwaride maalumu, alitoa hotuba hiyo akiwa amesimama na kwa ukakamavu mkubwa.
Lingine ni hotuba hiyo kusheheni takwimu ikiwa imebeba kila kitu ambacho Mtanzania alitaka kukisikia akionesha alivyotekeleza ahadi alizotoa Aprili 22, 2021 mbele ya bunge hilo alipohutubia kwa mara ya kwanza baada ya kukabidhiwa madaraka kuongoza Tanzania.
Hotuba yake imeweka msingi wa majadiliano unapotaka kuzungumzia miaka minne ya utawala wake kwa sababu unapotaka kujibizana lazima uwe na hoja na uwe na takwimu kuunga mkono au kupingana na kile unachokusudia.
Rais Samia ameweka kila kitu katika mizani yake kiasi kwamba yeyote hasa wale wanaopenda kusema ‘hakuna kitu kilichofanyika’ inabidi wajikaze hasa mbele ya jamii kuiaminisha kwamba hakuna kilichofanyika. Kimsingi, hoja hiyo haipo. Nimesema ni hotuba ya kihistoria kwa sababu ni rejea tosha unapotaka kuzungumzia miaka minne ya Rais Samia madarakani.

Ni rejea kwa kila eneo, kwa kila sekta, kwa kila jambo linaloihusu Tanzania kuanzia amani ya nchi hadi sekta ya michezo na sanaa akizigusa timu pendwa za Tanzania, Yanga na Simba.
Kwa kifupi, unaweza kusema bila ya kupepesa macho kwamba, Rais Samia amegusa na kuzungumzia kila kitu kinachogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania. Hayo ndiyo mambo aliyoahidi wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza.
Alichofanya Juni 27, 2025 ni kuueleza umma kwamba hakuwa anatania alipotoa ahadi katika kila eneo. Katika hotuba yake hiyo ya kuhitimisha shughuli za bunge, si tu ameeleza jinsi alivyofanikiwa karibu katika kila eneo, bali pia yale ambayo hajafanikiwa na hayo si kwamba hakuyafanyia kazi, isipokuwa yapo katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Haikushangaza hotuba yake imewagusa wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi ambao wamekiri kwamba ilijitosheleza na kueleza ukweli.
Mchambuzi na mtaalamu wa uchumi, Godvictor Lyimo anasema uchumi wa nchi umekua kama alivyoeleza Rais Samia katika hotuba yake. “Uchumi wa nchi umekua na kuna mambo mbalimbali yanaonekana kwa macho hata bila kuelezwa, tunaona barabara nyingi na majengo mengi ya kifahari yanajengwa ikilinganishwa na miaka iliyopita,” anasema Lyimo.
Anaongeza: “Uchumi katika miaka iliyopita ulikuwa ni 5.3 hadi 5.5, lakini sasa tumeona umekua hadi kufikia 5.6 haya ni mafanikio makubwa tuliyoyapata”. Anasema kilichochangia uchumi wa nchi ukue kwa asilimia kubwa ni sekta ya kilimo, miundombinu inayohusisha ujenzi wa vitu mbalimbali na sekta ya madini.
“Tunaona kilimo kimechangia Pato la Taifa kwa asilimia 26, ujenzi asilimia 12.8 na madini asilimia 10.1. Tunaiomba serikali iendelee kuboresha sekta ya kilimo ili iendelee kukuza uchumi, lakini kwenye suala la madini pia tumeshuhudia kuna migodi mingi mipya iliyochangia kukua kwa uchumi,” anasema.
Mdau wa masuala ya siasa, Hamida Kyulenzi anasema hotuba ilieleza mafanikio katika sekta zote muhimu kwa wananchi.
“Nimesikiliza hotuba kwa umakini na hotuba ilikuwa na mafanikio mengi hasa katika maeneo yanayogusa wananchi moja kwa moja. Naiomba serikali iendelee kuwekeza nguvu kwenye maeneo ya vijijini ili wananchi wa maeneo yale wanufaike zaidi, tumezoea kuona miradi mingi inatekelezwa mijini tu,” anasema Hamida.
Mtaalamu wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abel Kinyondo anasema Rais Samia amekuwa tofauti na marais wengine waliopita, na sifa kubwa aliyonayo ni kuendeleza miradi yote ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake.
Kwamba, pamoja na kupokea kijiti cha urais wakati ambao hakutarajia, hakutetereka, badala ya kuanzisha miradi yake ili kujipatia sifa binafsi, aliamua kuendeleza iliyoachwa. “Utakumbuka kauli ya utaona marais wote waliopita walianzisha miradi mipya na ile iliyoanzishwa ilitelekezwa hivyo kusababisha hasara, lakini yeye (Rais Samia) aliamua kumalizia na si kuanza moja,” anasema Profesa Kinyondo.

Anataja miradi hususani Daraja la JP Magufuli, Bwawa la Julius Nyerere, miradi ya barabara ya mwendokasi na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwamba endapo Rais Samia angeamua kuiacha ingesababisha hasara kubwa. Anasema miradi hiyo imetekelezwa kwa ufanisi na hakuna hasara ambayo ingeilazimu serikali kulipa wakandarasi kwa kusitisha mikataba ya ujenzi.
Hili la kuendeleza yaliyoanzishwa na watangulizi wake alilieleza vizuri Rais Samia katika hotuba ya Aprili 22, 2021 na ndio iliyozaa salamu yake maarufu ya ‘Kazi Iendelee’, akimaanisha kuwa pamoja na yote, lazima yaliyoanzishwa na marais na viongozi wengine yaendelezwe na kuanzisha mengine mapya.
Katika hotuba ya majuzi alieleza hili akisema, “Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa, tarehe 22 Aprili, 2021, takribani mwezi mmoja baada ya kushika wadhifa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nililihutubia Bunge hili.”
“Nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita. Vilevile, vipaumbele vilivyoainishwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020/2025,” anasema.
Anaongeza: “Niliahidi kudumisha mema ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mema mapya. Niliahidi pia kufanya mabadiliko pale itakapobidi kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija.”
Anasema maendeleo ni hatua, na licha ya kusikika mengi kutoka kwa mawaziri pamoja na wabunge kwa kazi iliyofanywa na serikali, “… lakini kwa kuwa mimi ndiye niliyetoa ahadi mbele ya Bunge hili, ninawajibika kutoa mrejesho hapa bungeni”.
“Ninafurahi kusema kuwa kipindi hiki kimekuwa ni cha kufanya mageuzi makubwa, kuongeza tija kwenye shughuli za kiuchumi, na kujenga msingi imara wa ukuaji endelevu, wenye kasi zaidi na unaowainua watu kiuchumi. Vilevile, kimekuwa ni kipindi cha kuimarisha ustahimilivu wa jamii, kukuza ustawi wa wananchi na kuwawezesha kujiletea maendeleo,” anasema Rais Samia.
Ni katika mrejesho huo, Rais Samia anawapitisha Watanzania katika kila hatua ya utekelezaji, kama ilivyoeleza awali akianza na umoja, amani, usalama na mshikamano wa kitaifa. “Kama ilivyokuwa kwa serikali za awamu zilizopita tumeshuhudia nchi yetu ikiendelea kujivunia tunu hizo na kuziimarisha.
Nyote ni mashahidi wa namna nchi yetu ya Tanzania imeendelea kuwa nchi moja na Watanzania wanaendelea kuwa wamoja, wenye mashirikiano licha ya kuwa na tofauti zao za kidini, mila na desturi, itikadi za kisiasa na hata ushabiki wa michezo (Simba na Yanga),” anasema Samia. Katika amani na usalama, alibainisha,
“Nchi yetu iko salama, mipaka yetu ipo salama na imara kwa sababu Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi yetu”.
Katika eneo hili Rais anazungumza kwa kina na kwa takwimu, uwezeshaji na uimarishaji wa majeshi ikiwamo Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi, Magereza, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Idara ya Uhamiaji, bila kusahau uratibu wa maafa.
Katika siasa na utawala bora, alizungumzia falsafa yake ya 4R akisema kwa kuongozwa na falsafa hiyo, “… ilituelekeza kwenye mageuzi, maridhiano, ustahimilivu na kujenga upya, na tuliweza kuwaleta wadau wa kisiasa na wengineo pamoja, na kufanya maamuzi na maboresho mbalimbali yaliyojumuisha na kushirikisha wadau wote”.
Hapa alizungumzia Tume ya Maridhiano iliyozaa na kuondoa mara moja zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, kutungwa kwa sheria mbalimbali za uchaguzi, asasi za kiraia kuwa huru shughuli zao na ahadi ya mchakato wa katiba mpya kuanza katika kipindi cha miaka mitano ijayo yaani 2025 – 2030.
Akazungumzia mapambano dhidi ya rushwa na Tanzania kupanda katika nchi zinazofanya vizuri kukabili tatizo hilo. Kuhusu Bunge, anawaambia wabunge: “Hakika mmefanya kazi kubwa kwani michango na ushauri wa Bunge hili umekuwa chachu kwa baadhi ya hatua tulizochukua kwenye mabadiliko ya kisera, kisheria na kiutendaji yaliyofanywa na serikali”.
Akazungumzia Uchaguzi Mkuu akiwapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na akagusia pia suala la uhuru wa habari, masuala ya uchumi ambako uchumi unakua kwa kasi na kufafanua kwa kina kuhusu deni la serikali na kuondoa upotoshaji unaosemwa.
Kwa kina Rais Samia alizungumzia kila sekta kwa upana wake na mambo yote mazuri yaliyofanywa na serikali yake tangu alipokabidhiwa madaraka, akitumia takwimu. “Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha, nisisitize kwamba utendaji wa serikali unapimwa kwa tathimini na takwimu.
Mimi nimetumia takwimu kueleza utekelezaji wa ahadi zetu kwa wananchi lakini ninyi wawakilishi wa wananchi mnafahamu vyema kilichofanyika katika maeneo yenu. Mwenye macho haambiwi tazama,” anasema Rais Samia katika hotuba hiyo.
Akawashukuru Watanzania kuanzia wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi hata wanasiasa kwa kuiunga mkono serikali. “Watanzania tumeendelea kudhihirisha uungwana wetu, hususani kwa kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa bidii na kwa moyo wa uzalendo,” anasema.


