Iran yasitisha ushirikiano IAEA

TEHRAN: RAIS wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameagiza kusitishwa kwa ushirikiano kati ya nchi hiyo na Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nguvu za Atomiki (IAEA), kufuatia mashambulizi ya Marekani dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran.
Uamuzi huo umefuata azimio lililopitishwa na Bunge la Iran, likitaka serikali kusitisha mara moja ushirikiano na shirika hilo la Umoja wa Mataifa.Hata hivyo, haijafahamika wazi hatua hiyo itaathiri vipi kazi za IAEA, ambalo limekuwa likifuatilia kwa karibu maendeleo ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Baada ya uamuzi huo wa Bunge, jukumu la kuhakikisha utekelezaji wake limekabidhiwa kwa Baraza la Juu la Usalama wa Taifa la Iran. Iran imekuwa katika mvutano wa muda mrefu na mataifa ya Magharibi kuhusu mpango wake wa nyuklia, huku Marekani ikihusishwa mara kadhaa na mashambulizi dhidi ya vinu vya nyuklia nchini humo.



