Wadau wahamasishwa vivutio vipya kuchochea utalii

DUBAI: Wadau wa sekta ya utalii nchini wamehimiza uboreshaji na ubunifu wa vivutio vipya vya kisasa ili kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.

Aidha, wamesisitizwa kuwa kutegemea vivutio vya asili pekee kama wanyamapori na fukwe hakuwezi kutosha kuipeleka Tanzania kwenye ushindani wa kimataifa wa utalii kwa miaka ijayo.

Akizungumza na HabariLEO kutoka  Dubai, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Disa Travels, Daud Lyon, amesema ni muhimu kwa Tanzania kufungua fikra na kuwekeza katika miradi mipya ya utalii ambayo inaweza kuwavutia siyo wageni wa kimataifa pekee bali pia Watanzania wenyewe.

“Tuna hazina kubwa ya asili lakini hiyo haitoshi. Tukiangalia mfano wa Dubai, walichagua kubuni vivutio vya kisasa licha ya kutokuwa na asili tuliyo nayo sisi, na sasa ni moja ya kitovu kikubwa cha utalii duniani,” amesema Lyon.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Bodi ya Utalii kutwaa tuzo mbalimbali za kimataifa katika tuzo za World Travel Awards, ikiwa ni uthibitisho wa juhudi zinazofanywa kukuza sekta hiyo.

Lyon amesema maendeleo ya utalii yana uwezo mkubwa wa kuinua sekta nyingine kama hoteli, usafiri na ajira, hivyo ni lazima serikali na sekta binafsi ziwekeze kwa nguvu zaidi, hususan katika kubuni vivutio vya kipekee na kuviwasilisha vizuri kwa dunia kupitia matangazo.

“Lazima tuelewe soko. Tusisite kutumia wasanii na wanamichezo maarufu kama mabalozi wa utalii wetu. Hii ni njia rahisi na ya haraka ya kuwafanya watu kufikiria Tanzania,” amesema.

Aidha, Lyon ametoa pongezi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi zinazoendelea kufanyika, lakini akatoa wito kwa wadau wote kuongeza kasi zaidi katika kufanya mageuzi ya kweli ya sekta hiyo.

mapato ya utalii yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka, huku idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania ikiongezeka kwa kasi kufuatia kampeni mbalimbali za kuitangaza nchi kimataifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button