Tuenzi Kiswahili, tukionee fahari

LEO ni maadhimisho ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani ambayo hufanyika kila Julai 7, tangu mwaka 2022 kutokana na azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO).

Ni siku ya kipekee kwa Tanzania ambayo tangu kupigania uhuru, Kiswahili kimekuwa lugha ya umoja, utamaduni na ukombozi.

Baada ya uhuru, imekuwa lugha ya taifa, ikiimarisha utambulisho wetu na kusaidia katika elimu, utawala na mawasiliano.

Sasa Kiswahili ni moja ya lugha 10 zinazotumiwa zaidi duniani, jambo ambalo ni la kufurahisha na la kujivunia kwa Watanzania.

Tunapongeza juhudi za serikali na wadau mbalimbali wanaoendelea kupaisha lugha hii kiasi cha kutangaza siku maalumu ya kuiadhimisha.

Kwa ushawishi wa Tanzania, Kiswahili sasa ni lugha ya kikazi katika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika kuadhimisha lugha hii kidunia leo, ni jukumu la kila Mtanzania ndani na nje ya nchi kuendelea kuenzi Kiswahili kwa kuitumia kwa heshima na kuhakikisha inaenea kimataifa.

Kwa ujumla, ipo haja kubwa ya kuendelea kuwekeza katika lugha hii adhimu kwa kuwa ni hazina ya taifa na chanzo cha utambulisho wa Mtanzania.

Kuenzi Kiswahili kuanzie kwa mtu binafsi kwa maana ya kutumia lugha kwa usahihi katika mazungumzo, mitandao, maandishi na katika vyombo vya habari.

Aidha, wazazi wawe mstari wa mbele kuhimiza watoto wao kuonea fahari lugha hii kuisoma na kuiandika kwa ufasaha. Tunatambua wazi kwamba katika utandawazi ambao dunia ni kama kijiji, ni jambo jema kujifunza lugha mbalimbali za kimataifa.

Lakini, wazazi wasikubali kutawaliwa na dhana potofu ya kuthamini lugha za kigeni pekee kwamba ndio usomi, usasa na maendeleo, na kukipa kisogo Kiswahili ambacho pia sasa ni lugha ya kimataifa.

Kwa hiyo, mikakati ya kuenzi lugha hii ihusishe shughuli za kiutamaduni kama vile utunzi wa mashairi, tamthilia, na vijana watumie mitandao ya kijamii kueneza misemo, nyimbo na maudhui ya Kiswahili.

Kwa upande wa taasisi, serikali iendelee kuweka mazingira mazuri kwa matumizi ya Kiswahili katika ofisi zake, matamasha na mikutano mbalimbali ya ndani na hata nje ya nchi.

Kwa muktadha huu, tunapongeza Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden chini ya Balozi Mobhare Matinyi kwa kushirikiana na jumuiya za Watanzania waishio nchini humo, kwa kuandaa na kufanikisha sherehe za maadhimisho Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani juzi jijini Stockholm.

Ubalozi umetekeleza kwa vitendo azma ya serikali ya kueneza na kukienzi Kiswahili duniani.  Kwa ujumla, kila mtu na taasisi, zikienzi na kukionea fahari Kiswahili kwani ni lugha yetu adhimu ya taifa na ya Umoja wa Afrika.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button