Mabaraza ya watoto yaundwe shuleni kisheria kukomesha ukatili

KATIKA kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa watoto vinakomeshwa kwenye jamii, serikali iliweka miongozo mbalimbali ya kuweza kupambana na vitendo hivyo. Moja ya miongozo hiyo ni kuundwa kwa mabaraza ya watoto katika shule za msingi na sekondari kwa lengo na kuwezesha watoto kueleza vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa.
Wadau wa kupambana na vitendo vya ukatili mashuleni likiwemo Shirika la World Vision Tanzania wanasema matukio mengi ya ukatili kwa watoto yanafanywa na wazazi au walezi. Hata hivyo watoto wenyewe nao wanakiri kuwa vitendo vingi hufanyiwa na wazazi wao, hasa vitendo vya kuozeshwa wakiwa wadogo, kuachishwa shule pamoja na kutumikishwa.
Uwepo wa mabaraza ya watoto katika shule za msingi na sekondari wadau wa kupiga vita vitendo hivyo wanayaona kama mwarobaini wa kupamba na vitendo hivyo kwa watoto. Endapo mabaraza hayo yataundwa watoto watajengewa uwezo wa kuzungumza, watakuwa huru kusema wanayofanyiwa na kuongeza usalama wao. Hata hivyo wazazi au walezi wengi ambao huwafanyia watoto vitendo vya ukatili, wamekuwa wakiwatishia hivyo wengi wa watoto ambao hufanyiwa ukatili wamekuwa wakiogopa kuzungumza.
Kukosa sehemu salama ya kutolea taarifa kwao kimekuwa kikwazo kikubwa cha kuendelea kupitia vitendo hivyo. Sehemu salama ambayo inatajwa kwa kiwango kikubwa ni katika mabaraza hayo, ambayo yanakutana na changamoto kubwa ya kuundwa lakini pia kukosa usimamizi shuleni.
Shule nyingi za msingi na sekondari nchini hazina haya mabaraza, hii ni kwa sababu hakuna mkazo wowote wa lazima kisheria kuunda mabaraza hayo. Aidha, hata katika shule ambazo yameundwa usimamizi wake umekuwa duni, kwani walimu wenye mafunzo ya kupokea kesi za matukio ya ukatili ni wachache.
Bado vitendo vya ukatili vinaendelea kutokea katika jamii, hasa maeneo ya vijijini ambako watoto wengi ni waoga, lakini pia uwezo wa kuyazungumzia hawana. Kutokana na mabaraza hayo kuonekana kuwa muhimu na yanaweza kukomesha vitendo hivyo, ni vyema serikali ikabadilisha mfumo wake wa kuundwa.

Nashauri serikali kwa kushirikiana na wadau kuanzisha sheria ambayo italazimisha mabaraza hayo kuundwa katika shule za msingi na sekondari lakini pia yapate walimu wa kuyasimamia. Kuletwa kwa sheria ya kuundwa kwa mabaraza hayo itasaidia kwa kiwango kikubwa kila shule nchini kuunda mabaraza hayo katika eneo lake na kuyatumia katika kupambana na vitendo hivyo.
Sheria pia izitake taasisi hizo kutafuta mwalimu maalumu wa kuyasimamia muda wote, ambaye atakuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za vitendo hivyo kutoka kwa watoto na jinsi ya kuwafundisha watoto kujiamini katika kutoa taarifa. SOMA: Ukatili wa Kijinsia Unaendelea Kuathiri Jamii
Tofauti na ilivyo kwa sasa mabaraza hayo kama ambavyo yanatajwa kuwa mwarobaini wa tatizo, wahusika ni vyema wakaona uwepo wa umuhimu wa sheria ili kuyafanya yafanye kazi inavyopaswa. Ushirikishwaji wa wadau katika kuundwa kwa sheria hiyo ni jambo muhimu zaidi kuhakikisha uwepo wa mabaraza hayo hauwezi kuathiri mfumo mzima wa kutolewa elimu shuleni. Katika shule ambazo mabaraza hayo yameundwa, ni vyema walimu na wanafunzi wakayatumia kuonesha mfano wa kukomesha vitendo vya ukatili katika jamii.



