Rose Muhando, Shusho, Bukuku watunukiwa tuzo

Katika tukio lililopambwa na sifa, vicheko na machozi ya furaha, waandaaji wa The Pinnacle of Mentorship & Excellence Awards (PIMEA) wameandika historia mpya kwa kutoa heshima kwa wanawake mashuhuri katika huduma ya kiroho na muziki wa Injili.
Hafla hiyo iliyofanyika Makumbusho ya Taifa, Posta – jijini Dar es Salaam, ambapo zaidi ya wanawake 15 waliopiga hatua kubwa katika kuwahudumia watu kupitia vipawa vyao walipewa tuzo maalum za heshima.
Mkurugenzi na mbeba maono wa tuzo hizo, Dk Christine Mbelwa, amesema lengo ni kuwatambua wanawake walioacha alama isiyofutika kwenye jamii kupitia huduma kama muziki wa Injili, mahubiri, na huduma kwa watumishi wa Mungu.
“Wanawake hawa wamevumilia, wamehudumu kwa moyo, na kazi yao imeigusa jamii kwa kiwango kikubwa. Tunataka kizazi kijacho kijifunze kuwa kuna wanawake waliotoa maisha yao kwa ajili ya huduma,” amesema Dk Christine kwa msisimko.
Miongoni mwa mastaa waliotunukiwa ni Rose Muhando, Pastor Bahati Bukuku, Christina Shusho, Upendo Nkone, Stella Joel Frank na Mama Imelda Maboya.
Viongozi wengine waliotunukiwa ni Askofu Tupilike Hans, Askofu Jane Muhegi, Dk Jennifer Mgendi, Dk Anny Fernandes, na Dk Gwantwa Mwakibolwa – wote wakitambuliwa kwa mchango wao katika kulijenga Taifa kiroho.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wake wa wachungaji maarufu nchini pamoja na waimbaji wa nyimbo za Injili waliopamba jukwaa kwa uimbaji wa kusisimua.
Katika hatua ya kusisimua, Dk Christine alimkabidhi mama yake mzazi, Bi Bernadetha Kanyankole, tuzo ya upendeleo kwa kuwa sehemu ya mafanikio yake na kwa mchango mkubwa wa kimalezi na kiroho.
“Tuzo hii ni ya kipekee kwa mama yangu ambaye amenilea katika msingi wa kumtumikia Mungu. Bila yeye, nisingekuwa hapa leo,” amesema Dk Christine kwa sauti ya hisia.
Kwa mara ya kwanza kufanyika, tuzo hizo zimepokelewa kwa kishindo na kupongezwa na mashabiki wa muziki wa Injili pamoja na waumini wa makanisa mbalimbali.“Ni mwanzo tu huu,” Dk Christine alihitimisha. “Tutakuwa tukitoa tuzo hizi kila mwaka — kadiri Mungu atakavyotuongoza!”



