Wakimbiaji zaidi ya 1,200 kushiriki Mbio kubwa za Ruaha

Zaidi ya wakimbiaji 1,200 Kushiriki Great Ruaha Marathon Season Five, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James asema ni chachu ya Utalii

IRINGA: Zaidi ya wakimbiaji 1,200 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki Great Ruaha Marathon Season Five itakayofanyika Julai 3 na 4 mwaka huu mkoani Iringa, huku Mwigulu Nchemba akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo kubwa la kimichezo na kitalii.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezindua rasmi maandalizi ya mbio hizo maarufu kwa jina la Great Ruaha Marathon Vibe Kitalii Season Five, akieleza kuwa imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kukuza utalii, michezo na uchumi wa wananchi wa mkoa huo.

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa utalii, wanamichezo pamoja na waandishi wa habari, huku ukionesha mwitikio mkubwa kutoka kwa jamii na sekta mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema mashindano ya mwaka huu yataendelea kuitangaza Iringa na vivutio vyake vya kipekee ndani na nje ya nchi, sambamba na kuleta fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi.

Alisema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii mkoani Iringa ikiwemo barabara ya Iringa–Msembe pamoja na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege Iringa hatua inayochochea utalii na biashara zinazohusiana.

RC James alisisitiza kuwa mbio hizo si tukio la michezo pekee, bali ni jukwaa pana la maendeleo linalounganisha sekta za utalii, uhifadhi wa mazingira, afya, michezo na uchumi wa jamii.

Aliwahimiza wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na tukio hilo kupitia huduma za malazi, usafiri, biashara ndogondogo na huduma nyingine, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na vyanzo vya maji vya Mto Great Ruaha Mkuu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), July Lyimo, alisema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza utalii wa ndani na nje ya nchi, hususan ukanda wa Kusini mwa Tanzania.

Alisema Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inaendelea kujitangaza kimataifa sambamba na juhudi za Serikali chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kupitia kampeni ya The Royal Tour, huku TANAPA ikilenga kufikia watalii milioni nane ifikapo mwaka 2030.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Sustainable Youth Development Partnership (SYDP) linaloratibu mbio hizo, Edward Athanas Milinga, alisema katika misimu minne iliyopita mbio hizo zimeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa mwamko wa utalii, kuimarika kwa juhudi za uhifadhi kupitia ushirikishwaji wa jamii pamoja na kukuza vipaji vya riadha kwa vijana.

Aliongeza kuwa tukio hilo limefungua fursa nyingi za kiuchumi na kijamii kwa wafanyabiashara, vijana na wananchi kwa ujumla, huku akiomba ushirikiano zaidi katika uhamasishaji na ushiriki wa taasisi mbalimbali.

Awali, Mratibu wa mbio hizo, Hamimu Kilahama, alisema msimu huu wa tano unalenga kupanua mafanikio ya misimu iliyopita kwa kuongeza ushiriki wa kimataifa na kukuza zaidi tasnia ya utalii kupitia michezo.

Uzinduzi wa Great Ruaha Marathon Season Five unaashiria hatua mpya ya maandalizi ya tukio hilo kubwa la kimichezo na kitalii, linaloendelea kuimarisha nafasi ya Iringa kama kitovu cha utalii na michezo nchini Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button