Mapato TRA kwa mwezi juu 77% miaka minne

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita makusanyo yake kwa mwezi yameongezeka kwa asilimia 77.

Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alisema hayo Arusha jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa tathmini ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo.

Mwenda alisema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani mwaka 2021, makusanyo kwa mwezi yalikuwa Sh trilioni 18.1 na wastani kwa mwezi walikuwa wakikusanya Sh trilioni 1.5.

“Leo miaka minne baadaye wastani kwa mwezi ni Sh trilioni 2.6 ambalo ni ongezeko la asilimia 77 ndani ya miaka minne,” alisema.

Mwenda alisema tangu kuanzishwa kwa TRA mwaka 1996, imekuwa ikivuka malengo lakini haikuwahi kutokea kuvuka mfululizo kila mwezi kwa miezi yote 12.

Alisema mwaka 1996, TRA ilikusanya Sh bilioni 531 kwa mwaka na wastani ulikuwa Sh bilioni 44.2 kwa mwezi na sasa miaka 29 baadaye wastani ni Sh trilioni 2.6 ambayo ni mara 61 ya mapato ya wakati inaanzishwa.

“Pia katika kipindi cha miaka hiyo tumeweza kuvuka lengo tulilopangiwa na serikali mara 10 tu na hii ni ya 10, mara ya mwisho kuvuka ni mwaka 2015/2016 kwa hiyo kitendo cha kuvuka mfululizo kila mwezi baada ya miaka minane lazima tuwapongeze watumishi waliopo na wafanyabiashara kwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari,” alisema Mwenda.

Alisema yote hayo yamewezekana kutokana na kuimarika kwa ushirikiano kati ya TRA, serikali na walipakodi na kwamba kufikiwa kwa malengo hayo hakumaanishi hakuna wakwepa kodi, bali wanafanya kazi kwa bidii kufanya mpango wa watu kulipa kodi kwa hiari kuwa endelevu.

Alisema tathmini waliyoifanya inaonesha huduma kwa walipakodi kwa kipindi cha mwaka uliopita zimeimarika na kuwasikiliza walipa kodi kumeongezeka kwa mikoa yote na wilaya zote.

“Mameneja na viongozi wengine kila Alhamisi ya kila wiki wao wenyewe wanatenga muda wa kusikiliza walipa kodi ili kutatua changamoto zao na hii imefanyika kwa mwaka mzima na imetusaidia sana na tutaendelea kufanya,” alisema Mwenda.

Alisema usimamizi wa watumishi wanaofanya kazi ndani ya TRA umeimarika, vitendo vya kusimamia maadili vimeongezeka na vitendo vya rushwa vimepungua lakini kwa wachache wenye kufanya vitendo hivyo wamekuwa wakizuia visitokee na kutoa elimu kwa watumishi na inapobidi wahusika huchukuliwa hatua ili visitokee tena.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button