Wafanyabiashara waguswa neema daraja la JPM

GEITA: WAFANYABIASHARA na wakulima mkoani Geita wamekiri kuwa baada ya kukamilika na kuzinduliwa daraja la JP Magufuli kumepunguza gharama za kuagiza bidhaa na kusafirisha mazao sehemu tofauti.

Wadau hao wa maendeleo wameeleza hayo katika mahojiano maalum na HabariLeo mjini Geita juu ya mapinduzi ya daraja la hilo katika sekta ya biashara na kilimo mkoani Geita.

Mmoja wa wafanyabiashara hao ambaye ni diwani wa kata ya Bukoli aliyemaliza muda wake, Faraji Self amesema daraja hilo limetengeneza tumaini jipya la kupanua uwigo wa kuuza na kusambaza biashara.

Ameongeza kuwa, daraja hilo ni mkombozi kwa wakulima katika kata ya Bukoli ambao ni wazalishaji wakubwa wa viazi na mihogo kwani limerahisisha usafirishaji wa mazao hayo kwenda jijini Mwanza.

“Kata ya Bukoli ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya mbogamboga na matunda, pamoja na mahindi na mpunga. Kwa hiyo daraja hili litaongeza kipato cha wakulima na wafanyabiashara”, amesema Faraji.

Naye Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa mtaa wa Kompaundi mjini Geita, Self Rajabu alisema daraja limeongeza muingiliano wa biashara kati ya Geita na mikoa ya jirani hususani Mwanza na Shinyanga.

Amesema kukamilika kwa daraja hilo inapngeza hamasa kwa wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa hiari kwa kuwa inadhihirisha kwamba pesa za wananchi zinatumika kwa ufasaha kwa manufaa ya umma.

Kwa upande wake mjasiriliamali kijana, Ramadhani Iddi amesema daraja hilo limewawezesha vijana waliojiajiri kusafiri ndani ya muda mfupi kwenda Mwanza kufuata bidhaa kuendelea na biashara.

Amesema kabla ya hapo walikuwa wanatumia muda mwingi kusubiri kivuko na kuwafanya watumie siku mbili na kupoteza muda mwingi pasipo kuendelea na biashara jambo ambalo ni tofauti na sasa.

Daraja la JP Magufuli lina urefu wa wa kilomita 3, pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 1.66 katika eneo la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza limekamilika kwa gharama ya sh bilioni 718.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button