Mtaalamu ataja visababishi homa ya ini

DAR ES SALAAM; DAKTARI wa Usalama Mahali pa kazi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group, Elias Birago ametaja sababu zinazoambukiza virusi vya homa ya ini na kuwataka wananchi kujitokeza kufanya vipimo na kupata chanjo ya ugonjwa huo.

Ametaja njia zinazoambukiza virusi vya homa ya ini kuwa ni kwa njia ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu mwenye maambukizi ikiwemo damu, jasho, maji ya uzazi “Amniotic fluid”, kujamiiana pamoja na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali vilivyotumika kwa mgonjwa wa homa ya ini.

Dk Birago ameyasema hayo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, ambapo wanapima virusi vya homa ya ini na kutoa chanjo ya ugonjwa huo.

“Lengo letu kubwa kutoa huduma hii katika maonesho ya Sabasaba ni kuikinga jamii isipate maambukizi ya homa ya ini, wale tutakaowapima na kuwakuta na shida tutawaelekeza namna nzuri ya kupata matibabu na kwa wale ambao wako salama watapata chanjo kupitia maonesho haya,” amesema Dk Birago.

Dk Birago amesema dalili za awali za ugonjwa huo zinaweza zisionekane lakini ugonjwa unavyoendelea mtu anaweza kupata manjano, mwili kuchoka, ngozi kuwasha, kupata homa, kupungua uzito hivyo kusababisha kushindwa kufanya kazi.

“Tumeweza kutoa elimu na umuhimu wa kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini kwa jamii kupitia maonesho haya kuiwezesha jamii kujua tatizo hilo kuwa lipo na halina dawa lakini lina kinga, iwapo mtu atafanya kipimo na kupata chanjo yake,”  alisema Dk Birago.

Amesema JKCI kupitia kitengo cha Usalama mahala pa kazi kilichopo Hospitali ya Dar Group wamekuwa wakitembelea taasisi na mashirika mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya ini.

Kwa upande wake Ofisa Uuguzi wa JKCI, Florah Kasema amesema wananchi waliotembelea banda la JKCI wamehamasika kupata chanjo hiyo ambayo wengi wao hawakuwa wakifahamu madhara yake.

Florah amesema ugonjwa wa homa ya ini unaongezeka kwa kasi na kuathiri jamii, hivyo wataalamu wa JKCI hawataishia kutoa huduma hiyo katika maonesho ya Sabasaba bali wataendelea kutoa elimu na chanjo hiyo katika vituo vyao vya afya.

“Ni muhimu wale wote walioanza kupata chanjo ya homa ya ini kuhakikisha wanamaliza chanjo hiyo kwa kupata chanjo zote tatu kwa kipindi cha miezi sita kama ambavyo wameshauriwa na wataalamu wa afya,” amesema Florah.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button