Mahakama Kuu yatupa maombi ya Lissu

DAR ES SALAAM; MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi ya mapitio yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, baada ya kubainika kuwa yaliwasilishwa kinyume cha sheria.
Lissu aliwasilisha maombi sita akiomba Mahakama iitishe jalada la kesi ya jinai inayomkabili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikihusiana na tuhuma za kuchapisha taarifa za uongo, ili lipitiwe na kuchambuliwa mwenendo wa shauri hilo lililoendelea Juni 2, 2025.
Katika maombi hayo, Lissu anapinga hatua ya Mahakama ya Kisutu kuahirisha kesi yake baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha ombi la kufichwa kwa baadhi ya mashahidi wake, akidai kuwa sababu hiyo haikuwa na msingi wa kisheria.
Akitoa uamuzi wake leo Julai 11,2025, Jaji Elizabeth Mkwizu alisema amepitia hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa maombi hayo yaliwasilishwa kinyume na Kifungu cha 372(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambacho kinazuia mapitio au kukatiwa rufaa dhidi ya amri ya kuahirisha kesi inayotolewa wakati shauri la msingi bado linaendelea.
“Kwa mujibu wa kifungu hicho, amri ya kuahirisha kesi haihitimishi shauri la msingi, hivyo haiwezi kukatiwa rufaa wala kufanyiwa mapitio. Kwa msingi huo, nayatupilia mbali maombi haya. Hata hivyo, mwombaji ana nafasi nyingine ya kuwasilisha upya maombi kwa kufuata utaratibu unaotakiwa kisheria,” alisema Jaji Mkwizu.
Awali, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, aliwasilisha pingamizi akidai kuwa maombi hayo hayakuzingatia taratibu za kisheria. Alidai kuwa amri ya kuahirisha kesi haikumaliza shauri na kwamba Jamhuri ilikuwa imewasilisha maombi rasmi namba 13298/2025 ambayo yangeathiri mwenendo wa kesi, hivyo kuomba ahirisho lilikuwa halali.
Pingamizi jingine lilitolewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema, aliyedai kuwa maombi ya Lissu ni ya mchanganyiko yaani maombi tofauti tofauti yameunganishwa bila kufuata utaratibu wa kisheria, na pia kwamba maelezo kwenye kiapo yanakinzana na yaliyomo kwenye maombi.
Aidha, upande wa Jamhuri ulisisitiza kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kufanya tafsiri ya kikatiba ya vifungu vya CPA kama ilivyoelezwa na mawakili wa utetezi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka inadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Tundu Lissu alichapisha taarifa za uongo kwa nia ya kupotosha umma kupitia mtandao wa YouTube.



