MOF mlezi wa mabinti, vijana kwa maendeleo chanya

MIRIAM ODEMBA FOUNDATION NI NINI?
MOF ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyowekeza kusaidia mabinti, watoto na vijana nchini Tanzania, iliyoanzishwa na mwanamitindo Mtanzania Miriam Odemba, anayeishi Ufaransa
Taasisi ya MOF, imejikita kutafuta suluhisho endelevu la changamoto zinazowakabili wanawake na watoto barani Afrika, hasa nchini Tanzania.

Lengo kuu la taasisi hii ni kuwawezesha wanawake na watoto kwa kuunga mkono mashirika, shule, na miradi iliyopo ambayo inalenga kuboresha maisha yao.
Mbali na kusaidia miradi ya kijamii, MOF pia inaunga mkono biashara za ndani kwa madhumuni ya kujipatia kipato hatua inayolenga kuhakikisha kuwa taasisi inakuwa endelevu kwa muda mrefu na kuendelea kutoa msaada bila kutegemea ufadhili wa nje pekee.

YALIYOTEKELEZWA NA MOF
1.Msaada kituo cha watoto yatima
Novemba 28,2021 mmiliki wa taasisi hiyo, Miriam Odemba alifika kutoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika kituo cha watoto yatima cha Salvation Army kilichopo Temeke.
Pamoja na zawadi mbalimbali, Miriam pia alipata chakula cha pamoja na watoto hao.

- MOF yatembelea wajasiriamali Mkuranga
Agosti 30, 2019, akiwa na taasisi yake, Odemba alifika wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuzungumza na wanawake wajasiriamali kuona namna ya kuwasaidia masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya maji waliyokuwa wakipitia kipindi hicho.

Katika safari hiyo, Odemba alichangia Dola 10,000 kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuongeza maji ambao unaendelea kusaidia wakazi wa eneo hilo hadi sasa.
- Atembelea Shule ya Msingi Mwongozo
Katika ziara yake shuleni hapo, aliyoifanya Oktoba 9, 2019, Wilaya ya Mkuranga, Odemba na taasisi yake alifanikisha ujenzi wa baadhi ya madarasa baada ya kuona idadi kubwa ya wanafunzi huku madarasa yakiwa machache.

“Mwongozo ina wanafunzi 900 ila ina madarasa saba tu, darasa moja linachukuwa wanafunzi hadi 100,” anasema Odemba.
Desemba 10, 2019 Wiki ya Maadhimisho Haki za Binadamu, MOF ilifika maeneo mbalimbali ya vijijini kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Hatua hii imekuwa endelevu kwa taasisi hiyo kufika maeneo ya vijijini kutoa huduma ya maji safi kwenye maeneo mengi nchini.
- Watoa msaada Sekondari Mtoro
AGOSTI 12, 2021, Shule ya Sekondari Mtoro iliyopo Dodoma likabidhiwa msaada wa sukari kilogramu 50 kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha pili na nne waliokuwa kambini kujiandaa na mitihani ya taifa.

5. Atembelea Sekondari Kibamba
Ziara ya OMF Shule ya Sekondari Kibamba ilikuwa ya hamasa na matumaini. “Kuona dhamira na ndoto za wanafunzi hawa wachanga hutukumbusha kwamba kwa usaidizi unaofaa, wanaweza kufikia chochote. Pamoja na Miriam Odemba Foundation, tumejitolea kuwawezesha vijana wa Tanzania kufikia uwezo wao wa juu,” Miriam anasema.

Wanafunzi Shule ya Sekondari Kibamba Dar es Salaam

- Atembelea wasichana Zanzibar
Katika tukio la International Super Model, Miriam alikutana na Asma Mwinyi Kusini mwa Unguja katika shule nne ambapo zoezi hilo lilioambatana na ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi 500.
“Tunashukuru sana watu wote walioshiriki nasi katika kufanikisha zoezi hili mpaka kufika hapa,” anasema Miriam.
- Atoa zawadi Dar es Salaam Girls Secondary

Februari 19, 2025 katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Miriam Odemba Februari 19, 2025 uongozi wa taasisi hii ilisherehekea siku hiyo pamoja na wanafunzi wa Dar es Salaam Girls Secondary School kwa kukata keki, kutoa zawadi mbalimbali, kutoa elimu na kuwahamasisha mabinti kupambania ndoto zao bila kukata tamaa.
- Wakabidhiwa cheti BASATA

Taasisi ya Miriam Odemba foundation ilikabidhiwa cheti cha utambulisho na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kama ishara ya shukrani kwa mchango wao bora katika sanaa na utamaduni wa Tanzania.
“Tunafurahia ushirikiano wetu na fursa nzuri ambazo ziko mbele yetu tunaposhirikiana kuleta mabadiliko ya kipekee,” inaaleza taarifa ya MOF.
Pamoja na hayo na mengine mengi, taasisi hiyo imekuwa ikijikita kutoa ushauri, uwezeshaji na kusaidia wasichana na wasiojeweza katika maeneo mbalimbali nchini.

KAZI ILIYOPO MBELE KWA SASA
1.Kutembelea wodi ya wazazi, kuchangia damu
TAASISI ya Miriam Odemba Foundation (MOF) inakusudia kufanya kampeni ya kuchangia damu, kutembelea wodi za wazazi na kutoa huduma zingine za afya Julai 25, jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya taasisi hiyo imeeleza kuwa lengo ni kusaidia wamama na kuchangia kwa namna tofauti kuwapa huduma za afya.
- MOF kuchangisha ujenzi vyoo Shule ya Mwendapole
Mkurugenzi wa Taasisi ya Miriam Odemba Foundation (MOF) Miriam Odemba anasisitiza Watanzania kuchangia fedha kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa vyoo na baadhi ya miundombinu katika Shule ya Misingi Mwendapole iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Hatua hiyo ni juhudi za taasisi hiyo katika kuiunga mkono serikali kuhakikisha wanafunzi wanapata miundombinu bora na imara ya kujisomea.
Odemba anasema lengo la taasisi yake ni kujenga vyoo 14 vipya, na kukarabati 12 kuhakikisha shule hiyo inakuwa na miondombinu bora.
“Kutuunga kwako mkono ni muhimu, kwani hakuna mchango mdogo wowote unahitajika kufanikisha hili,” anasema Miriam.



