Wananchi kupewa rushwa ni kudharauliwa na wagombea

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewataka wapigakura na wagombea kutopokea au kutoa rushwa hasa katika kipindi cha uchaguzi ili taifa lipate viongozi waadilifu, wazalendo na wenye nia njema ya kuwatumikia wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Crispin Chalamila akizungumza hivi karibuni alisema rushwa ni adui wa haki hivyo lazima ipigwe vita kwa nguvu zote ili taifa lipate viongozi bora na kuwataka wananchi kuepuka kuendekeza fedha ili kumpigia mtu kura.
Ni kweli rushwa ni adui mkubwa wa haki, hivyo nasi tunaendelea kusisitiza na kuunga mkono Takukuru kwa kuendelea kusimamia na kutoa elimu kwa jamii kuhusu kujiepusha na vitendo hivyo.
Jamii inapaswa kutambua kuwa Sheria ya kuzuia rushwa haibagui na iko wazi kuwa anayetoa na kupokea rushwa, wote lazima watachukuliwa hatua kwa sababu wote wamefanya kosa, hivyo wajihadhari wasijekuangukia katika mikono ya sheria hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kwa kupokea vitu ili wapigie kura viongozi.
Kumchagua mtu au watu unaowataka kuwa viongozi ni haki yako na wala hupaswi kulazimishwa ama kushawishiwa ili kuchagua.
Wananchi wanapaswa kuacha tabia ya kuthamini watu au mtu mwenye fedha kuwa ndio anaweza kuwapatia kitu fulani, lakini ukweli ni kuwa rushwa ni adui wa haki kwa sababu katika mazingira ya rushwa kwenye uchaguzi, inawanyima haki wagombea wengine wenye vigezo vyote kuwa viongozi kukosa uongozi kwa sababu hawana fedha ya kuwapa watu ili wawapigie kura.
Tunaamini wananchi wana uwezo na ufahamu wa kuchagua kiongozi kutokana na sera, ahadi, wasifu na mwenendo wa muomba kura bila kigezo cha fedha kwa sababu kuchagua kiongozi kwa sababu ya fedha ni kugeuzwa mtumwa, utawagharimu na kudhoofisha maendeleo ya nchi.
Tunapenda kuwakumbusha wapigakura mkichagua viongozi kwa rushwa na ukaja kuwa uongozi mbovu, basi mjue mtateseka nao miaka mitano na hamna la kuwafanya kwa sababu wameshinda kwa fedha zao na hakuna njia ya kurudisha nyuma uchaguzi.
Tunaendelea kuwakumbusha wananchi kuwa kura zao zina thamani kubwa katika mustakabali na maendeleo ya taifa hili, hivyo wasimame kidete kuwakataa wagombea watoa rushwa, kwa kukataa kupokea vitu ikiwemo nguo, vyakula na fedha kwa sababu kufanya hivyo ni kukubali kudharauliwa na wagombea hao.
Matumaini na imani yetu kwa Watanzania, uchaguzi mkuu wa mwaka huu utafanyika kwa haki na uwazi, kwa kusimamia na kuzingatia misingi ya uzalendo na kuweka maslahi mapana ya taifa mbele na kuachana na wagombea wasiostahili na watoa rushwa, kwa sababu madhara ya rushwa kwenye haki na maendeleo ya nchi ni makubwa, kataeni na kuichukia rushwa.



