Mikakati kukabili msongamano barabarani Dar izae matunda

WIKI iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliitisha kikaokazi cha viongozi na watendaji wa wilaya za Ilala na Kigamboni na wataalamu wa taasisi kadhaa kujadili changamoto ya msongamano wa magari.

Walihusika pia wakurugenzi wa halmashauri na Katibu Tawala wa Mkoa na wataalamu kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS), Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na Mamlaka ya Bandari (TPA). Lengo lilikuwa ni kutafuta suluhisho la kudumu la msongamano wa magari hususani malori.

Kitendo cha mkuu wa mkoa kuitisha kikaokazi hicho, kinadhihirisha serikali ilivyo na utashi wa kutatua kero hii ya msongamano kwa wananchi.

Tunatambua kwamba msongamano umechangiwa kwa kiwango kikubwa na ujenzi wa miundombinu ya barabara unaoendelea katika maeneo mbalimbali, ambao hata hivyo ni jambo la heri na la muda.

Hata hivyo, muda huu ambao ujenzi unaendelea, haupaswi kuchukuliwa kawaida kwa maana ya kuacha umma ukiendelea kuteseka na athari za msongamano unaochangiwa pia na wingi wa malori.

Kama ambavyo tafiti mbalimbali ziliwahi kufanywa na kutoa taarifa, msongamano wa magari una athari za kiuchumi, kijamii, kisaikolojia na kiusalama.

Wakazi wa Dar es Salaam wanapoteza muda mwingi ambao ungetumika kwa shughuli nyingine za kiuchumi. Matokeo yake, unapunguza uzalishaji wa kiuchumi na tija kazini.

Vilevile, unachangia gharama kubwa za usafiri kwa wenye vyombo vya moto binafsi kwa maana ya kutumia mafuta mengi. Wakati huohuo, watumiaji wa usafiri wa daladala wanalazimika kupanda pikipiki na bajaji, hali inayowalazimu kutumia fedha nyingi zaidi ya ambavyo wangepanda mabasi.

Kijamii, foleni zitokanazo na msongamano huathiri afya, ustawi na shughuli za kijamii za watu. Kusubiri kwa muda mrefu kwenye foleni pia kunachangia msongo wa mawazo na kuchoka kwa akili.

Kwa ujumla, msongamano unaathiri furaha ya watu kwa kuleta hisia za kuchoka na kukosa raha wakati wa kusafiri. Unaongeza pia uwezekano wa ajali kutokana na uendeshaji usiofaa hususani kwa pikipiki na bajaji ambazo wakati mwingine huingia kinyemela kwenye miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.

Ndiyo maana tunapongeza hatua ya serikali mkoani Dar es Salaam kuona umuhimu wa kujadiliana kwa kina kutafuta suluhisho tukiamini kikaokazi hicho kimeainisha mikakati sahihi na makini ya kuleta nafuu.

Ni matumaini yetu maazimio ya kikao yatatekelezwa kwa vitendo na bila kuchoka kunusuru umma wa wana Dar es Salaam na kero ya msongamano barabarani wakati wakisubiri suluhisho la kudumu ambalo ni kukamilika kwa miradi ya upanuzi na ujenzi wa barabara, ikiwamo za mwendokasi na usafirishaji zaidi wa mizigo kwa treni ya SGR badala ya malori.

Habari Zifananazo

One Comment

  1. Gᴏᴏɢʟᴇ ʜᴀꜱ ʙᴇᴇɴ ᴀɴ ɪɴᴄʀᴇᴅɪʙʟᴇ ᴏᴘᴘᴏʀᴛᴜɴɪᴛʏ! ᴇᴀʀɴ 𝟣𝟪𝟢𝟢+ ʙᴜᴄᴋꜱ ᴡᴇᴇᴋʟʏ ꜰʀᴏᴍ ʜᴏᴍᴇ! ᴀ ꜰᴇᴡ ᴍᴏɴᴛʜꜱ ᴀɢᴏ, ɪ ᴡᴀꜱ ꜱᴛᴜᴄᴋ ɪɴ ᴀ ʀᴏᴜᴛɪɴᴇ, ʙᴀʀᴇʟʏ ᴍᴀᴋɪɴɢ ᴇɴᴅꜱ ᴍᴇᴇᴛ. ɴᴏᴡ, ɪ ᴇᴀʀɴ 𝟤𝟢𝟧+ ᴀ ᴅᴀʏ ᴡᴏʀᴋɪɴɢ ꜰʀᴏᴍ ʜᴏᴍᴇ ᴡɪᴛʜ ᴄᴏᴍᴘʟᴇᴛᴇ ꜰʟᴇxɪʙɪʟɪᴛʏ! ɴᴏ ᴇxᴘᴇʀɪᴇɴᴄᴇ? ɴᴏ ᴘʀᴏʙʟᴇᴍ.
    ᴊᴏɪɴ ɴᴏᴡ➤➤ http://www.get.money63.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button