Waratibu INEC wapewa neno makundi Whatsapp

MTWARA: WARATIBU wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) katika mikoa ya Lindi na Mtwara wametakiwa kutojihusisha na makundi mbalimbali ya Whatsapp kipindi hiki wanapoelekea katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Hayo yamejiri leo Julai 17 wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu kwa waratibu hao yaliyofanyika kwenye Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.

Akizungumza kwa niaba ya Mjumbe wa INEC, Mratibu wa Mafunzo wa INEC, Cecilia Sapanjo amesema katika kipindi hicho cha mchakato huo wa uchaguzi wasijihusishe kutuma taarifa yoyote kwenye makundi hayo kwani kufanya hivyo ni kutenda kosa chini ya sheria na watawajibika kwa kosa hilo.

“Hivi sasa yapo magrupu mengi ya Whatsapp jitahidini katika kipindi hiki tuyapunguze ili tusije kukosea tukatuma taarifa yoyote katika magrupu haya,”amesisitiza Cecilia.

Mbali na hilo katika utekelezaji wa majukumu hayo wanapaswa kutoa taarifa mbalimbali kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili kuwajulisha wananchi na wadau juu ya mambo ya uchaguzi.

Pia amewasihi kuwa, iwapo watakuwa na uhitaji wa kutoa taarifa hiyo ni vema wakajiridhisha kabla ya kutoa taarifa lakini pia wahakikishe wanajiandaa kabla ya kukutana na vyombo vya habari.

INEC yaagiza mfumo shirikishi kuelekea uchaguzi mkuu

Kwa Upande wake mwenyekiti wa mafunzo hayo,  Daudi Muharangi amewasisitiza watendaji hao kuwa, watekeleze majukumu hayo vizuri kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za uchaguzi kuanzia sasa hadi mwisho wa zoezi hilo.

“Naomba niwasihi washiriki wenzangu kila mmoja kwa nafasi ya pekee tunaporejea tutambue kuwa tumesaini viapo kwahiyo tukavitekeleze, tukaviishi kwa kipindi chote tunapoenda kutekeleza kazi hii,”amesema Daudi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button