INEC yaagiza mfumo shirikishi kuelekea uchaguzi mkuu

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji na maofisa waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za uchaguzi mkuu 2025 kuendesha mchakato kwa mfumo shirikishi wa vyama vyote.

Aidha INEC imewataka watendaji na maofisa hao wa uchaguzi kusoma kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa ili kuweka usawa na haki.

Mjumbe wa INEC na Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari ametoa maelekezo hayo leo Julai 15, 2025 mjini Geita wakati akifungua mafunzo kwa watendaji na maofisa wasimamizi wa uchaguzi wa mikoa ya Kagera na Geita.

Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika mjini Geita kwa Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo, Maofisa Uchaguzi na Maofisa Ununuzi.

Amesema dhamana waliyopewa ya kusimamia na kuratibu, uendeshaji wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ni kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabari wa taifa hivyo wanapaswa kuwa waadirifu.

“Mjiepushe kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi, hakikisheni mnazingatia ipasavyo katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo”, amesema na kuongeza;

“Ajira za watendaji wa vituo, vizingatie kuajiri watendaji wenye weledi wanaojitambua, wazalendo waadirifu na wachapakazi, na kuachana na upendeleo kwa ndugu na jamaa ambao hawana sifa”.

Asina amesema hatua na taratibu za uchaguzi ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi kwa kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko na vurugu wakati wote wa uchaguzi.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Hidaya Gwando.

Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC, Hidaya Gwando amesema awamu ya kwanza ya mafunzo imehusisha vituo saba nchi nzima ambao kituo cha Geita kimeshirikisha washiriki 98 kutoka mikoa ya Geita na Kagera.

Mratibu wa Uchaguzi mkoa wa Geita, Herman Matemu amesema tayari mkoa umefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha watendaji na maofisa wa uchaguzi kutekeleza wajibu wao kwa ufasaha kwa mjibu wa sheria za uchaguzi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button