Uwezeshwaji wavuvi waongeza mavuno ya samaki

LINDI: SERIKALI imesema uwezeshwaji wa wavuvi wadogo umeongeza tija katika sekta ya uvuvi na kuongeza kiwango cha samaki kinachovunwa kwa mwaka kutoka tani 387,542.56 mwaka 2017/2018 hadi tani 529,668.01 mwaka 2024/2025.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena ametoa tathmini hiyo Julai 19, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake kwa awamu ya pili kwa mikoa ya Lindi na Mtwara iliyofanyika katika Bandari ya Lindi.

Alisema programu ya utoaji wa boti hizo za kisasa za uvuvi pamoja na programu nyingine zimelenga kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na shughuli za uvuvi hapa nchini.

“Zoezi la ugawaji wa boti za kisasa za uvuvi na vifaa vyake lililozinduliwa na Rais ni sehemu ya juhudi za serikali kuwawezesha wavuvi wadogo kunufaika na sekta ya uvuvi na juhudi hizi zimeongeza kiwango cha samaki wanaovunwa kutoka tani 387,542.56 zenye thamani ya Sh trilioni 1.74 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 529,668.01 zenye thamani ya Sh trilioni 4.5 mwaka 2024/2025,” alisema.

Meena alisema ongezeko hilo pia limeonekana kwenye mauzo ya mazao ya uvuvi nje ya nchi ambapo yameongezeka kutoka tani 44.939.79 hadi tani 59,746.41 sawa na ongezeko la tani 14,806.7.

Katika hatua nyingine, Meena amewataka wananchi waliokabidhiwa hizo za kisasa kukemea na kukataa vitendo vya uvuvi haramu kwani serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeanza kutumia teknolojia ya kisasa ya kudhibiti uvuvi haramu katika eneo la bahari kuu na maziwa ili kulinda rasilimali za uvuvi nchini.

“Ni matumaini yangu kuwa ninyi mnaokabidhiwa boti hizi hivi leo mtakuwa mstari wa mbele katika kukemea na kukataza vitendo vya uvuvi haramu. Pia nitoe rai kwa wavuvi wote nchini kuendelea kupinga vitendo hivi viovu, kwa pamoja tulinde rasilimali zetu kwa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa Idadi ya watu wanaojipatia kipato kupitia shughuli za uvuvi nchini imeongezeka kutoka watu milioni nne mwaka 2020 hadi kufikia zaidi ya watu milioni sita mwaka 2025 kutokana na uwezeshwaji wa wavuvi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya sekta ya uvuvi unaofanywa na serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Mohamed Sheikh alisema jumla ya boti 10 za uvuvi zilizokabidhiwa kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara zitawanufaisha wanufaika 427 kati ya hayo wanaume 391 na wanawake 36.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Nathalis Linuma alisema katika kuhakikisha wavuvi wanaunganishwa na taasisi za fedha, mkoa huo umeendelea kufanya usajili wa vikundi ili viweze kupatiwa mikopo ambapo hadi sasa jumla ya vikundi 8 vya ushirika wa wavuvi vimesajiliwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button