Wakandarasi Tanga watakiwa kumaliza kazi kwa wakati

TANGA; Wakandarasi wanaotekeleza mradi wa Hatifungani wa uboreshwaji wa miundombinu ya maji Jiji la Tanga, wametakiwa kuhakikisha mradi unakuwa wenye ubora na kukamilika kwa wakati
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Burian wakati wa hafla ya mapokezi ya vifaa vya miundombinu ya mradi huo vyenye thamani ya Sh Bil 6.3 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa).
Amesema kuwa mradi huo utasaidia kuleta tija kwa wakazi wa Jiji la Tanga na wilaya za jirani ambazo zinahudumiwa na mamlaka hiyo, hivyo ni muhimu utekelezwe katika viwango vinavyolingana na thamani halisi ya fedha lakini ukamilike kwa wakati.

“Mradi huu ni matumaini yangu utatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati, kwani ile ndoto ya Tanga ya viwanda inakwenda sambamba na upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika, “amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Uwasa, Mhandisi Geofrey Hilly amesema kuwa mradi wa hatifungani unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu na utasaidia kuongeza kiwango cha huduma ya maji kutoka lita Mil 45 hadi kufikia lita Mil 72..
“Mradi huu unakwenda kutoa huduma za maji katika wilaya za Tanga, Muheza, Pangani na Mkinga ambapo mradi kwa sasa umeweza kufikia zaidi ya asilimia 23,”amesema Mhandisi Hilly.

Mradi wa Hatifungani ambao utatekelezwa kwa gharama ya Sh Bil 53.1 unakwenda sambamba na kuboresha miundombinu ya maji, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na upandaji miti kwenye maeneo ya vyanzo ili kutunza mazingira.



