Samia apongezwa nguzo nne kuijenga nchi
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Rais Samia Suluhu Hassan anaongozwa na mambo makuu manne katika kusimamia maendeleo ya nchi na Watanzania kwa ujumla.
Ameyetaja mambo hayo kuwa ni pamoja na maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na kujenga upya Tanzania.
Aliyabainisha hayo juzi Dar es Salaam wakati wa Tamasha la Suluhu lililoandaliwa na Mwanamuziki Judith Wambura maarufu ‘Lady Jay D’ la kumpongeza Rais Samia tangu alipoingia madarakani kwa jitihada zake za kuijenga Tanzania mpya inayojali uhuru wa watu, demokrasia, usawa na haki za binadamu.
Kuhusu maridhiano, Nape alisema Rais Samia amefanikiwa kuwaleta Watanzania pamoja bila kujali tofauti zao za kisiasa na kuhakikisha utawala wa sheria, usawa, kutobaguliwa, fursa sawa kwa wananchi wote, kujiendeleza kibinafsi, jamii na taifa kwa ujumla zinafanyika.
Alisema katika utawala wake, Rais Samia anahakikisha kila mtu anafurahia haki zake za msingi na kutekeleza majukumu yake kwa uhuru kwa mujibu wa sheria bila kubughudhiwa.
Akizungumzia nguzo ya pili ya ustahimilivu, alisema Rais Samia anaamini katika ustahimilivu kwa kuhakikisha raia wa Tanzania wanapatanishwa na kupona kutokana na shida yoyote iliyokuwepo katika awamu zote za uongozi wa nchi hii ili wasonge mbele katika kuijenga Tanzania ya kesho.
Kwa mujibu wa Nape, Watanzania hawanabudi kukabiliana na changamoto za maendeleo kama taifa katika umoja na mshikamano na kuhakikisha nchi inasonga mbele kwa kujiamini.
“Mageuzi ya msingi na muhimu ya kiuchumi, kisiasa na (masuala ya) uchaguzi yatahakikisha sheria na haki nchini zinapatikana na kuhakikisha uchumi wa Tanzania unakua na kuzalisha ajira kwa watu wake. Mageuzi haya yanapaswa kuimarisha juhudi zetu kuelekea kuwa na jamii yenye haki, ustawi wa demokrasia na uchumi unaokua kwa faida ya Watanzania wote,” alisema Nape
Nape aliitaja nguzo ya nne inayotumiwa na Rais Samia kuwa ni ujenzi wa Tanzania mpya kwa kuhakikisha uchumi unakua na kuzalisha ajira za kutosha kwa vijana kama hali ya ustawi wa karne ya 21 inavyosisitiza kuwa maendeleo ni uhuru wa msingi.
Alisema ujenzi wa taifa ni mchakato unaohitaji uongozi unaoweza kuimarisha suluhu baini ya wananchi wote.
Mwanamuziki ‘Lady Jay D’, alimpongeza Rais Samia kwa kuleta suluhu nchini kutokana na kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi, dini au jinsi zao katika kuiongoza Tanzania.
“Mimi na mwenzangu Rama D, tumeandaa wimbo huu na kuzindua kampeni ya “Nasimama na Mama Samia” katika kuleta suluhu Tanzania ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo bila kujali itikadi zao, imani zao na kuhakikisha kuna uhuru wa kweli na demokrasia nchini,” alisema Lady JD.



