Wakulima wa kahawa kujengewa uwezo Kagera

BUKOBA: SHIRIKA lisilo la kiserikali linaloshughulika na maswala ya kilimo cha mazao, Cafe Africa, linatarajia kuwajengea uwezo na kutoa huduma za ugani kwa wakulima wa kahawa zaidi ya 35,000.
Lengo la kujengewa uwezo huo ni kufikia malengo makubwa ya kuzalisha kahawa yenye ubora nchini na kufikia malengo yaliyokubaliwa na nchi 25 zinazozalisha kahawa Afrika.
Katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa uzalishaji endelevu wa kahawa aina ya Robusta mkoani Kagera kwa awamu ya pili, Meneja wa Shirika hilo, Samora Mnyaonga amesema mradi huo kwa awamu ya kwanza ulifanyika Kagera mwaka 2020 hadi 2024 kwa lengo la kufufua mashamba mapya na kujenga uelewa kwa wakulima juu ya ubora wa kilimo cha kahawa.

Amesema kuwa mradi wa kwanza ulibadilisha fikira nyingi sana za wakulima hasa waliokuwa na mibuni ya miaka 100 hadi 200 shambani baada ya kubadili mtizamo wa kilimo cha kisasa na kubadili mibuni yao kufanya kuwa ya kisasa na Kupata mavuno mengi jambo ambalo lilivutia kaya nyingi mkoa wa Kagera na kuongeza kiwango cha mavuno kwa mwaka.
Amesema baada ya kufanya kazi kwa miaka mitano na Kuona mabadiliko makubwa wafadhili wa shirika hilo ambao ni wabobezi wa maswala ya kahawa ulimwenguni JDE Peet’s na Jacobs walivutiwa na sera za serikali mkoani Kagera juu ya kupunguza umasikini kupitia zao la kahawa na kuamua tena kufadhili mradi wa awamu ya pili kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.

Amesema utekelezaji wa miradi huu awamu ya pili unalenga kuongeza huduma za ugani mafunzo na uelimishaji juu ya uzalishaji wa kahawa,uongezaji wa thamani katika zao hilo pamoja na ushirikishwaji kuangiza ngazi ya kaya ,wadau hadi ngazi ya mkoa ili kupata zao bora la kahawa ambayo inahitajika sokoni
“Katika mradi huu tu tutaajili maafisa ugani wanaotoa huduma za ugani na ushauri 500,wakulima viongozi 300 mashamba darasan 300 , wataalamu wa kutoa ushauri watakaoungana na watafiti kutoa huduma kwa wakulima watafikia 200,”amesema Mnyonga.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa amesema kuwa amevutiwa na mipango ya shirika hilo kwani shirika hilo limeunga mkono juhudi mahususi za mkoa wa Kagera za kuhakikisha Kila mkazi wa Kagera ananufaika na kilimo cha kahawa bila kujali umri.
Amesema mkoa umefikia jitihada za makusudi za kuongeza uzalishaji hadi kufikia Tani 200,000 ifikapo mwaka 2030 ambapo kwa kuanza tu mkoa utawapitia vijana 10,000 maeneo ya kilimo kama sehemu ya kuwaongozea kipato
“Nalipongeza shirika hili kwa kuja na mpango mzuri wa kuunga jitihada za mkoa ,baada ya kuona kilimo cha kahawa Kinapesa mkoa umekuja na mkakati wa kutoa hekari moja moja kwa vijana 10,000 bila kuwahamisha makazi kwa kuwalimia ,kuwapa miundombinu,hatimiliki na Kila kitu hekari moja ili uwe urithi wa kudumu hata akiwa na familia lile shamba litakuwa lake na familia yake,” amesema Mwassa.

Meneja wa Bodi ya Kahawa mkoani Kagera, Edmond Zan kwa niaba ya meneja wa Bodi ya kahawa Tanzania TCB alisema kuwa Serikali nchini ilopata kiasi cha Sh Bilioni 537 zilizotokana na mauzo ya kahawa .
Amesema mikakati ya wadau inalenga kuwainua wakulima na kuongeza uzalishaji huku akisisitiza kuwa ni vyema wakulima wa Kagera wanatumia fursa hiyo vizuri hasa kuzingatia ubora wa kahawa ili kunufaika na soko la dunia .



