Wakandarasi waagizwa kufanya kazi usiku, mchana

KAGERA: WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa kimkakati upatikanaji wa miji katika miji 28 wa Rwakajunju Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera kubadili utendaji wake kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji kwa wakati.
Ametoa agizo hilo leo Julai 25, alipofanya ziara maalumu ya kukagua mradi wa kimkakati wa miji 28 uliopo kata Nyabiyonza Wilayani Karagwe Mkoani Kagera ikiwa ni sehemu ya kuangalia namna mradi huo unavyoendelea .
Amesema kuwa tayari serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia iliridhia kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo hivyo hakuna wakandarasi kuweka visingizio bali wachape kazi usiku na mchana ili kuwaondolea changamoto ya maji waliyokuwa nayo kwa muda mrefu wananchi wa Wilaya hiyo kwani huo ndio mradi pekee ambao utawaepusha na adha ya upatikanaji wa maji.

“Utendaji wa kazi lazima ubadilike kuanzia sasa hakikisheni mnafanya kazi usiku wa mchana na mradi huu ukamilike mwezi septemba mwaka huu kama Ambavyo tunakusudia kwa sababu lengo la serikali ni wananchi kupata maji Na kutumia muda wao kuzalisha,”amesema Aweso.
Amesema kuwa pamoja na mradi huo kutumia fedha nyingi lazima wakandarasi washughulikie changamoto za vibarua ikiwemo kuwapa mikataba ili kupunguza adha za vibarua hao wanatumika Kuharakisha kukamilika kwa mradi.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kalanga Laizer kuhakikisha anasimamia suala la vibarua ili vijana wasipate changamoto kupata maslai yao.

Aidha, amewasihi wasimamizi wa Mradi huo ambao ni mamulaka ya Maji na usafi wa mazingira Bukoba BUWASA kuhakikisha wanazingatia maagizo ya Rais Samia katika upande wa eneo la kutibu maji ili wananchi wapate maji safi salama na bora.
Mratibu wa mradi huo kutoka Buwasa Magreth Nyanga alisema mradi huo wa maji unagharimu zaidi ya Sh bilioni 60 ambapo ulianza kimkataba April 11, 2023 unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu.

Amesema kuwa mradi huo Kwa sasa umefikia asilimia 64 ambapo amemuhakikishia waziri juu ya usimamizi wa kazi hiyo kwa usiku na mchana ili uweze kukamilika na wananchi wapate maji safi na salama kwa wakati.
Mradi huo utakapokamilika unatarajia kunufaisha maelfu ya wananchi wa vijiji 13 kutoka Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera



