MOF yagusa maisha ya wagonjwa Muhimbili

DAR ES SALAAM: TAASISI ya Miriam Odemba Foundation imefanya ziara ya kugusa maisha ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kitengo cha watoto na wazazi, kwa kutoa mchango wa fedha na kusaidia mahitaji ya wahitaji waliolazwa hospitalini hapo.

Katika tukio hilo, mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Jengo la Watoto amesema kuwa kila Mtanzania anahimizwa kushiriki katika kusaidia wahitaji kadri ya uwezo wao, kwa kufuata utaratibu rasmi wa utoaji misaada hospitalini hapo.

“Sisi kama hospitali tunathamini sadaka na misaada kutoka kwa mtu mmoja mmoja au vikundi. Tunazingatia mfumo rasmi wa kupokea misaada ili kuhakikisha wahitaji wanafikiwa kwa usahihi,” ameeleza.

Mchango huo umetolewa kupitia moyo wa kujitolea wa taasisi hiyo inayoongozwa na mwanamitindo wa kimataifa mwenye Mtanzania, Miriam Odemba, ambaye kwa sasa anaishi jijini Paris, Ufaransa.

Miriam aliambatana na washirika mbalimbali wa taasisi yake, akiwemo msanii chipukizi wa muziki, Raykhan.

Akizungumza kwa njia ya simu, Miriam alisema: “Nimekuwa mwanamitindo wa kimataifa kwa miaka mingi, lakini moyo wangu upo nyumbani  Tanzania. Misaada kama hii siyo kwa ajili ya kujitangaza, bali ni hatua ya kuwahamasisha wengine kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu,”amesema.

Taasisi ya Miriam Odemba imekuwa ikiendesha kampeni maalum ya “Saidia na Miriam Odemba”, ambayo inalenga kuwafikia watu wenye uhitaji katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu na mazingira. Ziara hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imetoa hamasa mpya kwa taasisi na watu binafsi kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za kijamii.

Kwa upande wake, msanii Raykhan alisema kuwa ameguswa na moyo wa taasisi hiyo, na akaeleza:“Mara nyingi watu husubiri hadi tatizo litokee ndipo watoe msaada. Lakini tukio la leo limeonyesha kuwa msaada unaweza kutolewa kabla ya tatizo kuwa kubwa na unaweza kuokoa maisha.”

Aidha, Agness Maliki,  aliyeambatana na ujumbe huo, amesema kuwa tukio hilo limemfungua macho kuona kuwa mtu yeyote anaweza kushirikiana na hospitali kubwa kama Muhimbili bila hitaji la kuwa na fedha nyingi au taasisi kubwa.

“Nimejifunza kuwa hata mchango mdogo unaweza kumsaidia mgonjwa aliyekwama kulipia vipimo au dawa muhimu  jambo ambalo nilidhani linawezekana kwa watu wakubwa tu au mashirika makubwa,” amesema Agness.

Mchango uliotolewa uliwasilishwa kwa mujibu wa taratibu rasmi za serikali kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa malipo kupitia control number, kuhakikisha fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Taasisi ya Miriam Odemba Foundation inaendelea na miradi ya kijamii nchini, ikiwemo mradi wa ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Mwendapole iliyopo Kibaha, kama sehemu ya dhamira yake ya kuleta mabadiliko ya moja kwa moja katika maisha ya Watanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button