Mfumo wa ufundishaji mbashara kutumika sekondari nchi nzima
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema serikali imejipanga kuhakikisha mfumo wa ufundishaji mbashara unatumika katika shule zote nchini ili kumwezesha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi kwa wakati mmoja wakiwa katika mikoa tofauti.
Ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani, ambako alihimiza uwajibikaji kwa walimu na wanafunzi na kutembelea Kituo cha Smart Class kinachotumika kwa ufundishaji mbashara.
“Kibaha Sekondari ni mojawapo ya vituo vya mfano vya mfumo huu. Nilizindua rasmi majaribio yake jijini Dodoma kwa kuiunganisha Kibaha Sekondari na Dodoma Sekondari, na tuliona mafanikio yake. Sasa tunataka mfumo huu utekelezwe nchi nzima,”alisema Mchengerwa.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk Rogers Shemwelekwa kwa kusimamia vyema matumizi ya mfumo huo shuleni hapo na kumtaka aendelee kuiwezesha shule hiyo kuwa kituo bora cha mfano nchini.
Alisema iwapo miundombinu ya elimu itaendelea kuboreshwa shuleni hapo, serikali inaweza kufikiria kujenga chuo kikuu katika eneo hilo, ili kutimiza lengo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bora na ya kisasa.
Aidha, amempongeza mkuu wa shule hiyo, George Kazi kwa juhudi na mafanikio ya shule hiyo katika ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne na sita.
Hata hivyo, alimkumbusha kuwa jukumu hilo linaambatana na uwajibikaji, na kwamba akishindwa kutekeleza majukumu yake, hatua za kinidhamu zitachukuliwa.



