‘Uzazi wa mpango utafanikisha utekelezaji Dira 2050’

MWANZA : WATANZANIA wametakiwa kujiunga na huduma za uzazi wa mpango ili kuiwezesha nchi kutekeleza kwa ufanisi malengo mahususi yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kuhusu udhibiti wa kasi ya ongezeko la watu nchini.

Akizungumza na HabariLEO jijini Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), Dk David Kafulila amesema uzazi wa mpango ni moja ya nguzo muhimu zitakazoiwezesha Tanzania kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuimarisha uwekezaji katika rasilimaliwatu.

Kafulila amesema kasi ya ongezeko la watu nchini ni kubwa zaidi kuliko ya Afrika na dunia, hali ambayo inahitaji hatua madhubuti za kupanga familia kwa kutumia mpango wa afya ya uzazi unaotoa fursa kwa mume au mke kuwa na idadi ya watoto wanaoweza kuhudumiwa kutokana na rasilimali zilizopo.

Amefafanua kuwa kasi ya ongezeko la watu Tanzania ni zaidi ya asilimia tatu, ambayo ni kubwa kuliko kasi ya ongezeko la watu Afrika ambalo ni asilimia mbili na kasi ya ongezeko hilo kwa dunia ni asilimia moja. Hatahivyo  amesema  mataifa makubwa duniani kwa idadi kama China uamuzi wao wa kudhibiti watu kuzaliana kulisaidia kujenga rasilimali watu yenye ubora.

“Leo China ina ‘negative population growth’ (ukuaji hasi wa watu) na hata India ukuaji wake wa watu sasa ni chini ya asilimia moja,” alifafanua. Hatahivyo, hakusita kusema kuwa kwa kasi hiyo, Tanzania inakadiriwa kuwa na Watanzania milioni 140 ifikapo mwaka 2050.

Kafulila alisema kama ongezeko hilo lingekuwa sawa na wastani wa Afrika tangu dira ya kwanza ianzishwe, leo Tanzania ingekuwa na Watanzania milioni 56 badala ya milioni 68 na kufikia mwaka 2050 ingekuwa na Watanzania milioni 91 badala ya milioni 140. SOMA:fya Uzazi wa mpango unakupa raha, utaepuka karaha

 

Amesema ongezeko la watu kwa nchi maskini hugeuka kuwa mzigo badala ya faida kwa sababu ubora wake unakuwa mdogo kutokana na umasikini wa familia na uwezo mdogo wa serikali kumudu kuendeleza rasilimali watu. Kuhusu dhana kwamba wingi wa watu ni soko kubwa ni dhana potofu kwa madai kuwa soko hupimwa kwa kutumia uwezo wa kununua. Amesema ndio maana Ulaya ina asilimia saba ya watu duniani lakini ina asilimia 50 ya matumizi ya kijamiii ya dunia.

Amefafanua kuwa kama Tanzania ingekuwa na ukuaji wa watu sawa na wastani wa Afrika ina maana uchumi wa dola trilioni moja uliowezeshwa kwenye dira kufikiwa mwaka 2050 ungemaanisha wastani wa pato la mtu mmoja kuwa zaidi ya Dola za Marekani 10,000 badala ya lengo la sasa la Dola za Marekani 7,000.

Amesema kufikia Dira 2050 nchi inahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu na moja ya njia ya kufanikisha azma hiyo ni kwa serikali kuacha kuwekeza kwenye maeneo ambayo sekta binafsi inaweza kuwekeza ama moja kwa moja au kwa ubia ili kuiwezesha serikali kuwa na nguvu za kutosha za kuwekeza kwenye rasilimali watu. Amesema watu wengi lakini wasio na ubora wa maarifa na afya hawawezi kuleta tija katika uchumi wa nchi bila kuwa na mipango inayotoa majawabu ya ongezeko la idadi ya watu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button