Teknolojia ya ubebeshaji inavyoipa sifa Tanzania uzalishaji wa korosho

TEKNOLOJIA bora ya ubebeshaji inayotumika kuzalisha zao la korosho nchini Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa nchi nyingine za Afrika kujifunza kupitia wataalamu wabobezi waliopo.

Kutokana na uwepo wa wabobezi hao hivi karibuni wadau mbalimbali wa korosho kutoka nchi nane za Afrika zinazobangua korosho waliwasili nchini kwa lengo la kujifunza teknolojia mbalimbali zinazotumika kuzalisha korosho ikiwemo ya ubebeshaji.

Akizungumzia teknolojia hiyo na namna inavyotumika Mtafiti wa Kitengo cha Uhaulishaji wa Teknolojia na Uhusiano wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara, Gaspar Mgimiloko anasema ziko nchi nyingine za Afrika ambazo zinatumia teknolojia hiyo lakini Tanzania ina wataalamu wabobezi zaidi ikilinganishwa na nchi hizo.

Wadau wa korosho kutoka nchi nane za Afrika zinazolima na kubangua korosho wakiwa katika shamba la Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI)-Naliendele mkoani Mtwara kujifunza kwa vitendo teknolojia bora ubebeshaji inayotumika kuzalisha zao hilo. (Picha zote na Sijawa Omary)

Mgimiloko anafafanua hayo alipozungumza na gazeti la HabariLEO hivi karibuni na kusema anapozungumzia suala la ubobezi wa wataalamu anarejea uwezo wa mtu mmoja katika kubebesha miche na kuifanya ikue na kuzalisha. Anasema Tanzania ina wataalamu wenye uwezo wa kubebesha takribani miche 500 kwa siku yenye uwezo wa kuchipua na kuendelea kuota kwa asilimia 96 mpaka asilimia 98.

“Wakati kuna wengine wakibebesha miche karibu nusu ya miche aliyobebeshwa inakufa lakini wataalamu wa Tari wamefanikiwa kutoka hatua moja kwenda nyingine ambayo ni asilimia 96 mpaka asilimia 98 miche ya mikorosho hiyo inapona,” anasema Mgimiloko.

Kwa upande wake aliyekuwa Mtafiti Mkuu wa Zao la Korosho wa kituo Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Naliendele, Profesa Peter Masawe anasema Tanzania imekuwa ikifanya vizuri katika zao la korosho kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uwepo wa kituo hicho, wataalamu wa kutosha, ardhi na mambo mengine.

“Katika mambo ya utafiti Tanzania ndiyo inaongoza, tunafurahi tu kwamba unapowafundisha wenzako unaona wanakuuliza kitu ambacho wewe umeshajifunza miaka ishiriki iliyopita, kwetu ni furaha wanajua tuko mbele na watatangaza jina letu,” anasema Masawe.

Mkuu wa Idara ya Ubanguaji wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ambaye pia ni Mratibu wa mafunzo hayo, Mangile Malegesi anasema katika mafunzo hayo yaliyotolewa na bodi hiyo kuhusu teknolojia za uzalishaji korosho amejifunza hatua mbalimbali za uandaaji wa korosho katika hatua za awali ikiwemo ubebeshaji.

Pia, anasema wamepata nafasi ya kutembelea mashamba ili kujionea wakulima wao wanavyofanyia kazi ujuzi walioupata kutokana na mafunzo waliyopatiwa na wataalamu hao ili waone namna ambavyo wanatumia mbinu walizopewa katika uzalishaji.

Anasema washiriki wa mafunzo hayo kutoka ndani na nje ya nchi wameonesha kufurahishwa na namna CBT
na serikali kwa ujumla inavyowekeza katika uzalishaji bora wa zao la korosho.

“Wenzetu waliokuja kututembelea kutoka nchi hizo nane ikiwemo Tanzania wamevutiwa sana namna ambavyo bodi ya korosho au serikali ya Jamhuri ya Muungano ilivyowekeza kwenye korosho na namna mikakati ilivyowekwa kwa ajili ya zao hili, tunaimani kupitia haya mafunzo wataalamu wetu kutoka Tanzania watapata uzoefu kutoka kwa wenzao na kubadilishana uzoefu,”anasema Malegesi.

Katika hatua nyingine washiriki wa mafunzo hayo walipata nafasi ya kujifunza kwa ubebeshaji kwa vitendo kupitia mtaalamu Mgimiloko ambaye anasema moja ya sababu ya kutumia njia hiyo ya ubebeshaji kwenye uzalishaji ni kupata korosho ambazo ni sawa na mti mama kwani wakipanda mbegu kuna uwezekano ikabadilika na kuwa tofauti na mti mama.

“Sababu ya pili ni kwamba njia hiyo inafupisha muda wa kuanza kuzaa kwani ikibebeshwa mkorosho unaanza kuzaa mapema lakini uko mbele mti wa korosho uliyopandwa kikawaida na ule uliyobebeshwa kwenye mavuno hakuna utofuti inazaa sawa kwa hiyo tunachofata hapo kubebesha ni kuwa na miti yenye uzaaji,” anasisitiza Mgimiloko.

Kwa upande wao baadhi ya wadau waliyoshiriki mafunzo hayo wakiwemo wakulima, watafiti, wabanguaji na wafanyabiashara wameonesha kufurahishwa na mafunzo hayo huku wakieleza kunufaika nayo. Mshiriki kutoka Tanzania, Jane Fagache anapongeza teknolojia hiyo bora na kusema ni njia bora kwa sababu inaufanya mmea kukua kwa haraka na kuleta manufaa zaidi katika uzalishaji wa korosho.

“Kupitia elimu hii tunaenda kuwahimiza wakulima watumie njia ya ubebeshaji kwa sababu mazao yatakuwa mengi zaidi, mimea itakuwa bora zaidi na ukulima kwa sasa utakuwa rahisi kuliko ilivyokuwa kabla ya kutumia njia hii, kwa kweli tunaipongeza sana serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa jitihada za kuendelea kuliimarisha zao la korosho,” anasema Jane.

Mshiriki mwingine, Huruma Kilakuno mkazi wa Dar es salaam, Tanzania anasema njia hiyo ya ubebeshaji ni
bora na endapo itatumika vizuri uzalishaji utaongezeka na kuinua uchumi wa wakulima kupitia zao hilo.

“Wenzetu wa nchi nyingine za Afrika zile nane wamekuja hapa wameshangaa sana kwamba sisi tuko mbele sana katika hili eneo na wamejifunza na sisi pia tulipata uzoefu kutoka kwao na naamini kwamba kwa ushirikiano huu zao la korosho na sekta hii, zitasonga mbele,” anasema Huruma.

Nchi zilizoshiriki mafunzo hayo ni Rwanda, Kenya, Zambia, Sudan Kusini, Uganda, Malawi, Msumbiji
na Tanzania ambayo ni mwenyeji wa mafunzo hayo ya siku tano yaliyofanyika mkoani Mtwara kwa lengo la
kuongeza mnyororo wa thamani katika zao la korosho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button