RC Katavi Aonya Kupandisha Bei

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewataka wafanyabiashara mkoani humo kutochukua kipindi cha baada ya uchaguzi kama kisingizio cha kupandisha bei za bidhaa, akisisitiza kuwa shughuli za biashara ziendelee kama kawaida na bidhaa zenye bei elekezi ziuzwe kwa viwango vilivyowekwa rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mrindoko amesema huduma zote muhimu kama elimu, afya, usafiri, biashara, masoko, na vituo vya mafuta zinapaswa kuendelea kutolewa bila usumbufu wowote ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata mahitaji yao ya kila siku bila changamoto.
Amesema serikali haitavumilia kuona baadhi ya wafanyabiashara wakitumia visingizio vya kisiasa au mabadiliko yanayotokana na kipindi cha uchaguzi kuongeza bei kiholela, jambo ambalo linaweza kuathiri maisha ya wananchi.

Ameongeza kuwa ofisi yake itaendelea kufuatilia hali ya upatikanaji wa bidhaa na huduma muhimu ili kudhibiti ongezeko holela la bei na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa gharama nafuu. Aidha, RC Mrindoko ameishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa pamoja na vyombo vingine vya dola kwa kuhakikisha Katavi inabaki kuwa eneo salama na lenye amani.
Amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo hivyo katika kulinda usalama wao na mali zao, akisisitiza kuwa utulivu na mshikamano ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi mkoani humo. SOMA: TRA yapania kuboresha huduma kwa wafanyabiashara



