Fyekeo la kwanza CCM

HAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza wanachama wake waliotia nia ya kuwania ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na viti maalumu ambao wamepita katika mchujo wa awali baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kukutana jijini Dodoma.

Wakati wabunge wapatao 30 wakiwa wametemwa katika mchujo huo wa awali, kwa upande wa wabunge waliobaki baadhi wanakabiliwa na mchuano mkali katika kura za wanaCCM ngazi ya kata na jimbo.

Akizungumza kabla ya kuanza kutangaza majina hayo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinzudi (CCM), Amos Makalla alisema kamati imehakikisha inatenda haki.

Wabunge waliotemwa
Miongoni mwa wabunge ambao wametemwa katika mchujo wa awali (majimbo) ni Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Luhaga Mpinga (Kisesa), January Makamba (Bumbuli), na Vedastus Manyinyi (Musoma Mjini).

Wengine ni Emmanuel Ole Shangai (Ngorongoro), Mohammed Monni (Chemba), Nicodemas Maganga (Mbogwe), Lazaro Nyamoga (Kilolo), Zuberi Kuchauka (Liwale), George Mwenisongole (Mbozi), Flatei Massay (Mbulu Vijijini), Pauline Gekul (Babati Mjini), Christopher Ole Sendeka (Simanjiro).

Wengine walioenguliwa ni Idd Kassim (Msalala), Seif Gulamali (Manonga), Shaban Shekilindi (Lushoto), na Yahya Khamis (Kijini), Cecil Mwambe (Ndanda) ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa Chadema, Angeline Mabula (Ilemela), Godwin Kunambi (Mlimba), Stephen Byabato (Bukoba Mjini), George Ruhoro (Ngara), Vedastus Manyinyi (Musoma Mjini).

Wengine ni Geoffrey Mwambe (Masasi), Mansour Shanif Hirani (Kwimba), Hassan Kungu (Tunduru Kaskazini), Iddi Mpakate (Tunduru Kusini), Iddi Kassim (Msalala), Alfred Kimea (Korogwe Mjini) na Twaha Mpembenwe (Kibiti).

Wengine walioachwa ambao ni mara yao ya kwanza kuwania ni Rais wa Klabu ya Soka ya Yanga, Hersi Said aliyewania jimbo la Kigamboni na Makamu wa Rais wa Klabu ya Yanga, Arafat Haji aliyewania ubunge jimbo la Shaurimoyo Kisiwani Unguja.

Wakongwe watia nia
Hata hivyo, katika orodha ya watiania kwenye majimbo, wamo wakongwe kwenye siasa waliowahi kuwa wabunge ambao wanawania katika majimbo mbalimbali.

Nao ni Mary Nagu, Assumpta Mshama, Peter Serukamba, Fuya Kimbita, Charles Tizeba, Kangi Lugola, Nyambari Nyangwine, Aggrey Mwanri, Stephen Masele, Lazaro Nyalandu, William Ngeleja, Peter Msigwa na Angellah Kairuki

Mchuano mkali

Miongoni mwa majimbo yenye ‘vita’ kali baina ya watiania wa ubunge watakaopigiwa kura za maoni katika ngazi ya kata na jimbo ifikapo Agosti 4, ni Kinondoni ambako mtifuano ni baina ya mbunge wa zamani, Idd Azzan, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa TFF, Michael Wambura na mbunge wa sasa, Abbas Tarimba.

Jimbo lingine linalotarajiwa kuwa na mtifuano ni Iringa Mjini ambalo mbunge wa sasa, Jesca Msambatavangu atakabiliana na Mchungaji Peter Msigwa aliyewahi kuwa mshindani wake akiwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kabla ya kuhamia CCM.

Jimbo la Makambako pia linategemewa kuwa na ‘vita’ kali kati ya Mbunge wa sasa, Deo Sanga (Jah People) na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.

Haki imetendeka
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla alisema: “Kamati imehakikisha inatenda haki. Lakini pia kwa wale ambao hawatapata nafasi niwaombe waendele kuwa watulivu, waendelee kutoa ushirikiano ni wanachama wazuri na wametimiza haki yao ya kikatiba”.

Alisema, “Chama Cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za kutumikia katika chama chetu, inawezekana ukakosa udiwani, ukakosa ubunge, lakini ukachanguliwa kuongoza ndani ya chama.”

Aliongeza: “Wingi wa wanaCCM waliojitokeza inathibitisha pasi na shaka kuwa CCM ni chama pendwa na ni chama kinachokubalika, kinategemewa na kuwa hatima ya uongozi wanakitegemea Chama Cha Mapinduzi.”

Kura kwenye kata, majimboni
Waliopitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa iliyokutana Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma sasa wanakwenda kwenye kibarua kingine cha kampeni za ndani ya chama kuomba kura kwa wanaCCM ngazi ya kata na jimbo, kampeni ambazo zimepangwa kuanza leo hadi Agosti 3, 2025.

Walioomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watapigiwa kura za maoni katika ngazi ya kata na jimbo ifikapo Agosti 4, mwaka huu.

Wagombea wa ubunge viti maalumu (Tanzania Bara) na wagombea ubunge na uwakilishi wa viti maalumu (Zanzibar) watapigiwa kura ya maoni kwenye Mkutano Mkuu Maalumu ya mikoa ya UWT ifikapo Julai 30, mwaka huu.

Hata hivyo, Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itakutana Agosti 22, mwaka huu kwa ajili ya kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa jimbo na viti maalumu ikiwa ni siku tano kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufunga dirisha la utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa ubunge na udiwani.

Watakaopitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa ndio watapeperusha bendera ya CCM kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Agosti 27, 2025 itakuwa ni siku ya Tume kufanya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani. Kampeni zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28, mwaka huu kwa Tanzania Bara na Oktoba 27 mwaka huu kwa Zanzibar ili kupisha kura ya mapema.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button