Watumishi wa umma kutahiniwa kupanda daraja, kuthibitishwa kazi
KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka amesema serikali inaboresha utaratibu wa utumishi wa umma kwamba ili mtumishi apande daraja au athibitishwe kazini atalazimika kufanya mtihani kupima uwezo wake.
Aidha, amewataka watendaji kuacha tabia ya kuwakataa watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi zao au kutaka kuwahamisha.
Ameonya pia kwamba watumishi wenye changamoto au matatizo ya kiutendaji wasihamishiwe kwenye taasisi nyingine bali wabaki katika taasisi walizopo na kuadhibiwa ndani ya taasisi husika.
Ametoa kauli hiyo katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa watendaji wakuu wa taasisi za umma 114 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi.
Balozi Kusiluka alisema mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watendaji hao na kuwapa fursa ya kubainisha changamoto, jinsi ya kuzishughulikia na kuishauri serikali.
“Nimeongea na Katibu Mkuu Utumishi (Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), mtumishi mwenye matatizo asihamishiwe kwenda taasisi nyingine bali aadhibiwe ndani ya taasisi aliyoko,” alisema Balozi Dk Kusiluka.
Aliongeza: “lakini pia viongozi msiwakatae watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi zenu, wengine wanabadilika kutokana na makosa yao na mnapowakataa, hata nyie mngekataliwa.”
Kauli hiyo iliungwa mkono na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi aliyesema baadhi ya changamoto za watendaji wa taasisi ni kuwakataa baadhi ya watumishi wanaohamishiwa kwenye taasisi zao.
“Changamoto nyingine ni wakuu wa taasisi wanawakataa watumishi, wanasema simtaki huyu, wanadai hawajui utendaji wao walipotoka, sasa wewe umewekwa katika taasisi hiyo kwa kuwa umeonekana unafaa ndio utatue changamoto za hao watumishi,” alisema Mkomi.
Alitoa mfano, “Alishakuja kiongozi mmoja akasema nusu ya watu wangu (watumishi) hawafai na aka-recomend (akatoa maoni) wabadilishwe. Nilishangaa sana, hadi leo nashangaa…halafu yeye bado ni kiongozi…nikamwambia na wewe taarifa yako imekuja, ninayo ya kuwa haufai.”
Alisema katika utumishi kiongozi anapaswa kuwa na ujuzi wa kuwaongoza watu wake na kutambua uwezo wao kwani watumishi hawawezi kufanana, kila mmoja ana tofauti.
Aidha, aliwataka watendaji hao kuwa na uhusiano nzuri na bodi za taasisi hizo na si kwa kuwahonga, bali wabadilishe mtazamo juu ya utendaji wao kwa kujifunza vitu vipya sambamba na kuwafanya watumishi ndani ya taasisi zao kuwa na amani ili kujenga mazingira bora ya kazi yenye kuzaa ufanisi.
Balozi Kusiluka alisema serikali inaboresha utaratibu wa mfumo wa utumishi wa umma huo ili uwe na tija zaidi kwa watumishi kwa kuwapima uwezo wao kabla ya kuthibitishwa kazini au kupanda daraja.
“Tunataka mtumishi akiajiriwa kabla ya kuthibitishwa afanye mtihani na hata kabla ya kupanda daraja apimwe uwezo wake, ili anapomsimamia ‘junior’ (mwenye uzoefu mdogo) awe na uhalali,” alisema Balozi Dk Kusiluka.
Aliongeza: “Maana si mtu anaitwa Senior Officer (Ofisa Mwandamizi) au Principal (Ofisa Mwandamizi Mkuu) lakini hawezi hata kuandika dokezo au huwezi kumtuma kwenda kutoa mada mahali… hili si sawa, lazima tupime uwezo wao kabla ya kupanda daraja.”
Katika hatua nyingine Balozi Dk Kusiluka aliwapa watendaji hao malengo sita mahususi ili kuleta tija na ufanisi katika taasisi wanazoziongoza ili kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikali kuu.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, alisema anatarajia kuona taasisi za umma zenye
mwelekeo wa kibiashara zinaongeza ufanisi wa kiutendaji, mapato na faida na hivyo kupunguza utegemezi
wa ruzuku kutoka serikali kuu.



