Rose Tweve na Nancy Nyalusi wapata ushindi wa kishindo ubunge UWT Iringa

IRINGA: Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Iringa imeandika historia nyingine baada ya kuwasafishia njia wabunge wa viti maalumu, Rose Tweve na Nancy Nyalusi kurejea bungeni kwa ushindi wa kishindo katika kura za maoni zilizofanyika leo.
Katika mchuano uliotawaliwa na ushindani mkali, Rose Tweve alijihakikishia nafasi ya kwanza kwa kura 554 huku Nancy Nyalusi akimfuata kwa karibu kwa kura 507.
Mafanikio haya yanawafanya wawili hao kuwa miongoni mwa wanawake wachache waliodumu kwenye siasa kwa ujasiri na ushawishi mkubwa.

Mhandisi Fatma Rembo, ambaye alikuwa akitajwa kuwa tishio na chaguo la wengi kutokana na rekodi yake ya kiuongozi na ushawishi kijamii, ameangukia nafasi ya tatu baada ya kujizolea kura 326, matokeo yaliyoacha gumzo katika ukumbi wa kura na mitandao ya kijamii.
Kinyang’anyiro hicho kilichovuta hisia za wanachama na wadau mbalimbali wa siasa, kilihusisha wagombea nane waliopigiwa kura na jumla ya wajumbe 851.

Wengine na kura zao kwenye mabano ni pamoja na Seki Kasuga aliyepata kura 152, Maria Makombe 59, Tumaini Msowoya 31, Lydia Nzema 25, huku Scola Mbosa akijizolea kura 8 pekee.
Wachambuzi wa siasa wameeleza kuwa ushindi wa Rose na Nancy unadhihirisha namna walivyoweza kujenga misingi imara ya kisiasa na uhusiano wa karibu na wanachama wa UWT, huku wakisisitiza kuwa ushindani ulioshuhudiwa ni ishara ya uimara wa demokrasia ndani ya chama.

Kwa sasa macho yote yanaelekezwa kwa Kamati Kuu ya CCM, ambayo itafanya uteuzi wa mwisho.



