Tiba upandikizaji moyo Kuanzishwa JKCI

DAR ES SALAAM; TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imeanza mikakati ya kupanua huduma zake ikiwa ni pamoja na kuanzisha huduma ya upandikizaji moyo.
Kutokana na hali hiyo imeunda na kuzindua kamati maalumu yenye wataalamu 10 itakayokuwa chini ya uenyekiti wa Dk Evarist Nyawawa, ikihusisha pia wataalamu wa kada mbalimbali ambao watasimamia uratibu wa mkakati huo.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo Julai 31, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge wakati akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo Septemba mwaka 2015.

“Kwa kutumia wataalamu waliopo, taasisi imejipanga kuanza kufanya maandalizi ya upandikizaji wa moyo ili kufikia miaka mitano ijayo Tanzania iwe inafanya upandikizaji wa moyo.
“Leo tunapoenda kuadhimisha miaka 10 tunaenda kufungua kamati maalum itakayokuja kufanya kazi kwa miaka mitano kufanya kazi ya upandikizaji moyo, haya ni mafanikio makubwa sana kama taasisi kupandikiza moyo,” amesema.
Amesema nchi zinazofanya upandikizaji wa moyo Afrika ni pamoja na Afrika Kusini, Misri na baadhi ya nchi za Afrika Kaskazini, hivyo kwa hatua hiyo itakuwa nchi ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Uhitaji ni mkubwa,magonjwa ya moyo yanaongezeka kwa kasi na vijana wanapata hasa magonjwa ya misuli ya moyo, ambapo moyo unakuwa umechoka na ukiwa uko chini ya miaka 50 kwa nini upoteze maisha mapema, ndio maana sisi kama taasisi tunataka kulinda afya ya wananchi waweze kutibiwa,”amesisitiza Dk Kisenge na kuongeza;

“Tunavyo vifaa vilivyowekwa hapa ni vikubwa ambavyo serikali imewekeza kwenye vifaa vikubwa vinavyoendana na nchi zilizoendelea kama Marekani, Uingereza na zingine na hospitali kubwa 20 duniani zinakuja kufanya huduma hapa wanakuja kwa sababu ya maendeleo ya rasilimali watu na vifaa vilivyowekezwa na serikali,”amefafanua.
Dk Kisenge amesema sasa taasisi hiyo imeweza kufanya upasuaji wa kubadilisha valvu bila kupasua kifua ambapo huduma hizo zinatolewa na hospitali kubwa pekee.
“Matibabu ya moyo Duniani kote ni gharama valvu kuwekewa ni Sh milioni 10 na kuzibua mishipa ni Sh milioni sita kwa hiyo ni hela nyingi na serikal imefanya kazi kubwa asilimia 75 wanabima ya afya na sasa serikali imepitisha bima ya afya kwa wote sasa watu wote watapata huduma,”amesema.

Ameeleza kuwa serikali pia ina utaratibu wa kutoa msamaha wa matibabu ambapo JKCI kila mwezi inatoa msamaha ya zaidi ya Sh milioni 200.
Amewashukuru wadau mbalimbali wa benki na mashirika ya umma, kwani kwa kipindi cha mwaka jana walitoa kiasi cha Sh bilioni 2.7 ambayo imeenda kusaidia wasio na uwezo.
Dk Kisenge amesema magonjwa ya moyo yanasababishwa na mtino wa maisha usiofaa kama unywaji wa pombe uliokithiri ,kutofanya mazoezi, kutokula kula vizuri, uvutaji wa sigara uliokithiri na kuwataka watanzania kufanya mazoezi.



