TAMWA yazindua mradi wa ufugaji nyuki

DAR-ES-SALAAM : CHAMA cha Wanawake Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) kimezindua mradi mpya wa ufugaji wa nyuki katika Kijiji cha Msufini, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, ukiwa na lengo la kukuza uchumi wa jamii na kulinda mazingira dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza jijini Dar-es-salaam katika mafunzo maalum kwa Wanachama wa TAMWA kuhusu ufugaji wa nyuki, Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho, Dk. Rose Reuben, amesema mradi huo unalenga kuwawezesha wakazi wa Msufini, hususan wanawake na vijana, kupata chanzo mbadala cha mapato kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.

“Tunatarajia kuwa na mizinga 200 ya nyuki katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu. Mbali na kuongeza kipato kwa familia, mradi huu utasaidia pia kuhifadhi mazingira kupitia matumizi ya nyuki katika misitu na bustani,” alisema Dk. Reuben.

Kwa mujibu wa Dk. Reuben, mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi kutekelezwa mwezi Agosti 2025 baada ya kukamilika kwa mafunzo ya awali na usambazaji wa mizinga na vifaa vya msingi kwa wanufaika. SOMA: Hongera Tamwa, TCRA, asante Rais Samia

Aliongeza kuwa tayari TAMWA imeanza kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa ajili ya msaada wa kitaalamu na vifaa muhimu kwa utekelezaji wa mradi huo. “Tunaendelea kuwahimiza wadau na wafadhili kuunga mkono juhudi hizi ili kupanua mradi na kuwafikia walengwa wengi zaidi,” aliongeza Dk. Reuben.

Kwa upande wake, Afisa Nyuki, Christina Samweli, aliwafundisha washiriki namna ya kutambua asali halisi, akieleza kuwa: “Asali halisi inaweza kuhifadhiwa hadi miaka miwili bila kuharibika. Unaweka maji kwenye chupa, kisha unamimina asali. Ikiwa inazama chini, hiyo ni halisi. Ikiwa inapanda juu, basi si halisi.”

Naye Afisa Michechemuzi wa TAMWA, Florence Majani, alisema mradi huo umejikita katika kuwawezesha wanawake na vijana kujiajiri, kuongeza kipato cha kaya, na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na mashirika yanayosaidia maendeleo ya jamii. “Faida za mradi huu ni nyingi: ajira, uzalishaji wa asali, uhifadhi wa mazingira na maarifa ya matumizi endelevu ya rasilimali asilia,” alisema Majani.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button