Teknolojia za kisasa kuongeza tija uzalishaji mazao

MOROGORO: WAKULIMA wameshauriwa kutumia mbinu bora za Kilimo ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kilimo hifadhi kinacholinda mazingira na kuimarisha mavuno.
Mtaalamu wa kilimo kutoka Kampuni ya Mzuri na Agram Afrika, Salimu Msuya amesema hayo wakati wa utoji elimu ya matumizi ya teknolojia za kisasa za Kilimo mjini Morogoro.
Msuya amesema kilimo hifadhi kinajumuisha mbinu za kupunguza usumbufu wa udongo, kuacha masalia ya mazao shambani, kutumia mazao funika hasa jamii ya mikunde ili kurutubisha udongo, pamoja na kufanya kilimo cha mzunguko au mseto.
Pia amewashauri watumie pembejeo za kisasa zikiwemo mashine za kisasa zinazolenga kuwaongezea tija kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ili kuongeza kupato chao na kwa Taifa.
Msuya amesema moja ya teknolojia iliyobuniwa ya Mzuri Pro-Til inayofanya kazi nyingi kwa pamoja kama kulima uwekaji mbolea, upandaji na kufukia mbegu kwa wakati mmoja na hivyo kuokoa muda, gharama na kulinda afya ya udongo.
Amesema teknolojia hiyo ni sehemu ya kilimo stahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kwani inapunguza mmomonyoko wa udongo na kulinda bioanuwai ya udongo.
Amesema mashine hiyo Inachangia uhifadhi wa maji na hewa safi, Inapunguza utegemezi wa mbolea za viwandani kwa kuongeza rutuba asilia.
Msuya amesema teknolojia ya mashine hiyo inafaa kwa mazao mbalimbali kama mahindi, alizeti, kunde, ngano, na mengineyo huku ikipunguza kwa kiwango kikubwa uchakachuaji wa udongo unaosababisha kuharibika kwa ardhi.
Wakati huo huo wakulima wa zao la Pamba Kanda ya Mashariki inayojumisha mikoa ya Iringa, Pwani , Tanga , Kilimanjaro na Morogoro wameongeza kiwango cha uzalishaji kutoka wastani wa kilo 800 kwa ekari hadi kufikia wastani wa kilo 2,700.
Ofisa Kilimo Mwandamizi wa Bodi ya Pamba Kanda ya Mashariki, Alphonce Ngawagala amesema hayo baada ya Kanda hiyo kutoa mkulima bora kitaifa wa zao hilo aliyezalisha kilo 2,723 kwa ekari .
Ngawagala amesema mkulima huyo ,ni Alfa Bushiri kutoka kata ya Mwaya, wilaya ya Ulanga , mkoani Morogoro ambaye alivuna kilo hizo kwa ekari baada ya kufuata kanuni bora za kilimo cha zao hilo.
Amesema kiujumla msimu uliopita wastani wa uzalishaji wa pamba ulikuwa ni watani wa kilo 500 hadi 800 ekari na kwa msimu mwa mwaka huu uzalishaji umeongezeka baada ya utolewaji elimu ya kwa wakulima juu ya kuzingatia kanuni bora za kilimo cha pamba.



